Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Hasunga - Msimu Ujao Korosho Kununuliwa Kwa Kujisajili Kupitia Mfumo Wa ATMIS
Sep 21, 2019
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_47180" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utaratibu utakaotumika kwenye msimu wa ununuzi wa korosho 2019/20  kwenye ofisi za wizara hiyo Jijini Dar es Salaam.[/caption]

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo

Serikali imetangaza ununuzi wa korosho wa msimu mpya   unaohusisha teknolojia ya wanunuzi kujisajili kwenye Bodi ya Korosho kupitia mfumo wa Wizara ya Kilimo wa kusimamia Biashara za Kilimo (Agricultural Trade Management Informataion System – ATMIS).

Imeeleza pia kuhusu deni la korosho msimu uliopita  inalodaiwa na wakulima wakubwa kuwa shilingi bilioni 50, ambalo linaendelea kulipwa kila siku kulingana na shehena ya korosho zinazonunuliwa na wanunuzi.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Tarehe 20 Septemba 2019 Jijini Dar es Salaam.

“Msimu wa 2019/2020 mfumo wa ununuzi wa korosho utakuwa kwa njia ya mnada wa wazi kwa kutumia jukwaa la Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) ambapo hakutakuwa na matumizi ya masanduku ya mnada,”alisema Waziri.

Amesema kuwa wanunuzi watakaosajiliwa na kukidhi vigezo watatakiwa kulipa Kinga ya Dhamana (Bid Security) kutegemeana na kiasi cha korosho mnunuzi anachotaka kununua kupitia kwenye akaunti ya usuluhishi inayomilikiwa na Soko la Bidhaa.

“Mfumo huu utaruhusu wanunuzi mbalimbali kutoka maeneo mbalimbali duniani kushiriki katika mnada. Wanunuzi wa nje ya nchi wataweza kushiriki katika mnada moja kwa moja na hawatalazimika kufungua makampuni hapa nchini,” alisema Waziri.

Amesema badala yake wanunuzi hao watadhaminiwa na benki za malipo (Settlement Bank) zinazotambuliwa na Soko la Bidhaa (TMX) hivyo kuongeza ushindani katika minada.

“Benki za malipo zitawajibika kutoa uhakikisho wa uwepo wa fedha kwa ajili ya malipo ya korosho kwa mujibu wa taratibu za soko,”alisema.

Akizungumzi kuhusu wanunuzi wa ndani na nje ya nchi alisema wataruhusiwa kununua korosho  ghafi kwa mafungu (stakes) kati ya tani 50 mpaka tani 500 kulingana na mahitaji.

“Korosho hizo katika mafungu (stake) zitapangwa kulingana na vigezo vya ubora na daraja.  Kiwango cha korosho kitakachouzwa katika kila kikao (mnada) kitatokana na taarifa zilizopo katika katalogi ya mauzo,” alisema.

“Mnunuzi atalazimika kununua kiasi chote cha korosho kilichopo katika fungu katika kikao kimoja  ili kuwezesha utoaji wa korosho katika ghala kwa kutumia utaratibu wa korosho za kwanza kuingia ndizo za kwanza kutoka (first in, first Out- FIFO),”alifafanua Waziri.

Alisema Wanunuzi wenye leseni watapewa msimbo (code) maalumu watakazozitumia kuingia kwenye mfumo na kushiriki katika minada. Mnunuzi atakaeshinda katika mnada atawajibika kulipia korosho alizoshinda ndani ya siku tatu (3) baada ya mauzo kufanyika.

Malipo yote yatafanyika kupitia benki za malipo (Settlement Bank) zinazotambuliwa na Soko la Bidhaa. Soko la bidhaa litawalipa wadau wote kwa mujibu wa sheria ndani ya siku mbili tangu mnunuzi kukamilisha malipo husika.

Waziri alieleza  kuwa utaratibu huu utaondoa ulazima wa wanunuzi kusafiri kutoka eneo moja kwenda lingine ili kushiriki minada ya korosho.

“Minada ya mauzo ya korosho itafanyika siku mbili kwa wiki katika maghala yote kulingana na upatikani wa korosho, minada itakuwa siku ya Jumanne na Alhamisi,” alisema.

Waziri Hasunga amesema lengo la utaratibu huu mpya ni kupanua wigo wa soko ambao wanaamini utaongeza chachu ya ushindani na kuwezesha bei nzuri zaidi kupatikana kulingana na mwenendo katika soko la dunia.

Kupitia jukwaa la Soko la Bidhaa kutakuwa na wigo mpana kwa wanunuzi, kutakuwa na uwazi wa bei za korosho na wakulima watalipwa haraka zaidi na kwa wakati.

Alisema lengo la Serikali ni kuona wakulima wote wanalipwa fedha zao moja kwa moja  kwenye akaunti zao binafsi katika Benki zilizopo katika maeneo yao ya uzalishaji.

“Msimu wa ununuzi wa korosho Mwaka 2019/2020 kwa sasa umefunguliwa rasmi. Katika msimu wa 2019/2020 tunategemea kuzalisha tani 300,000 za korosho ghafi kutoka tani 224,000 zilizozalishwa 2018/2019 ikiwa ni ongezeko la asilimia 34%,” alisema Waziri.

Alibaiisha kuwa Wizara ina mikakati mbalimbali ya kuongeza uzalishaji ikiwa ni pamoja na Kuhamasisha matumizi sahihi ya viutilifu bora na  kuhakikisha upatikanaji wa viuatilifu hivyo kwa wakati na kwa bei nafuu pamoja na kutoa mafunzo kwa wakulima.

Waziri alisema  kuwa  matumizi sahihi ya viuatilifu yataongeza tija miongoni mwa wakulima kutoka wastani wa kilo 10 kwa mti kwa mwaka hadi kufikia kilo 35 kwa mti kwa mwaka.

Alisema Wizara yake kupitia Bodi ya korosho imeongeza maeneo mapya yanayolima korosho kutoka mikoa mitano ya awali ambayo ni Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani na Tanga na kufikia mikoa 17.

“Mikoa mingine inayolima korosho kwa sasa ni Dodoma, Singida, Tabora, Mbeya, Iringa, Kilimanjaro, Katavi, Morogoro, Songwe,Kigoma, Njombe na Shinyanga,”alisema.

Katika musimu wa mwaka 2018/2019 serikali iliamua kununua korosho zote toka kwa wakulima kutokana na kuyumba au kushuka kwa bei ya korosho katika soko la minada.

“Hatua hii ilikuwa ni ya dharura iliyochukuliwa ili kulinda maslahi ya mkulima, kuanza mkakati wa kubangua korosho zote hapa nchini, kufufua viwanda vya kubangua korosho vilivyopo na kuongeza ajira kwa watanzani,”alisema.

 Lengo la Serikali ya Tanzania chini ya Rais John Magufuli ni kuhakikisha kuwa wakulima wananufaika na mazao yao na kupata bei nzuri kulingana na mwenendo wa soko.

Bei ya korosho ghafi katika Mwaka 2018/2019 iliyotolewa na wanunuzi ilikuwa ndogo sana, ikilinganishwa na bei ya Msimu wa 2017/2018.

Utekelezaji wa maamuzi na maagizo hayo ulifanywa kwa ushirikiano mkubwa kati ya wizara ya kilimo, viwanda na biashara, wizara ya  Ulinzi na Jeshi la kujenga taifa, TAMISEMi, na wizara ya mipango na Fedha.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi