Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam
Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian, Mhe. Vicky Ford ameonesha kuridhishwa na utoaji wa huduma katika kituo cha afya EngenderHealth Tanzania kilichopo Yombo Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Ford ameoneshwa kuridhishwa na utoaji wa huduma jumuishi kwa familia, mama, watoto, vijana na watu wenye ulemavu wakati alipofanya ziara katika kituo hicho Tanzania ambacho kinafadhiliwa na Serikali ya Uingereza.
“Nimeridhika na utoaji wa huduma katika kituo hiki hasa baada ya kuongea na akina mama, vijana na watu wenye ulemavu kwa nyakati tofauti maelezo yao kwangu yanaonesha huduma ni nzuri na zinaridhisha,” amesema Waziri Ford.
Pia nimeona mazingira ya kituo hiki pamoja na kuongea na Madaktari, Wauguzi na watoa huduma kwa kweli wamenifariji kazi yao ni nzuri na nawaomba waendelee kufanya kazi kwa bidii bila kuchoka, ameongeza Waziri Ford
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa EngenderHealth Tanzania, Dkt. Moke Magoma ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa ufadhili wa baadhi ya huduma katika kituo hicho na kuahidi kuwa wataendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi katika kuwahudumia Watanzania wanaotumia kituo hicho.
“Mheshimiwa Waziri kwa niaba ya wafanyakazi wa kituo hiki, tunakushukuru sana kwa ufadhili wa huduma za wahanga wa unyanyasaji na Watoto na Watu Wenye Ulemavu, huduma hii imekuwa na msaada mkubwa sana katika jamii, tunakuahidi kufanya kazi kwa bidii na weledi,” amesema Dkt. Magoma.
Baadhi ya wakina mama waliokuwa katika kituo hicho kwa ajili ya matibabu na huduma mbalimbali wameomba kuongezewa watumishi ili kupunguza msongamano wa wagonjwa pamoja na kujengewa kituo jumuishi ambacho kitaweza kusaidia upatikanaji wa huduma zote katika eneo moja.
Kituo cha EngenderHealth Tanzania kanafadhiliwa na Serikali ya Uingereza katika huduma za mama, mtoto, vijana na wenye ulemavu hasa wahanga wa unyanyasaji wa kijinsia na unyanyasaji wa watoto.
Huduma nyingine zinazotolewa kituoni hapo ni pamoja na huduma jumuishi kwa familia, mama, Watoto, vijana na wenye ulemavu.
Waziri Ford yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 3 - 5 Aprili, 2022.