Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Dkt. Mabula Ataka Ufanyike Upembuzi Mashauri ya Ardhi Yaliyokaa Muda Mrefu
Oct 06, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula ameagiza ufanyike upembuzi kwa mashauri yote ya ardhi yaliyokaa muda mrefu kutokana na sababu zisizo na mashiko.

Amemtaka Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya, Stella Tullo kusimamia agizo hilo kwa kumpatia taarifa mapema mwezi Novemba 2022.

Aidha, alimtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuangalia kwa jicho la tatu Mabaraza yote ya Ardhi ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuwa kumekuwa na malalamiko mengi ya mlundikanao wa kesi za muda mrefu.

Dkt. Mabula alitoa agizo hilo Oktoba 6, 2022 wakati wa Kikao kazi cha Kitengo cha Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kilichofanyika jijini Dodoma.

Dkt. Mabula alisema, Serikali inatambua umuhimu na michango ya mawakili katika kuvisaidia vyombo vya utoaji haki na kuwakumbusha mawakili suala la maadili ya kiutendajI hasa kwa baadhi ya wajumbe kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Kwa mujibu wa Dkt. Mabula, uzoefu unaonesha mashauri mengi yanayowakilishwa na mawakili ndiyo yenye kuchukua muda mrefu kumalizika.

‘’Mashauri mengi ya ardhi katika mabaraza hayapewi kipaumbele na Wakili anaweza kupanga tarehe ya kesi ambayo kwa siku hiyo ana mashauri katika vyombo vingine vya kutoa haki", alisema Dkt. Mabula.

Waziri wa Ardhi aliongeza kwa kusema kuwa, uchunguzi wa awali unaonesha pia baadhi ya mapingamizi yana dhamira ya kupoteza muda hususan yale mashauri yanayohusu taasisi za fedha.

‘’Mashauri mengi yanayofunguliwa na wananchi walioshindwa kurejesha mikopo  kwa wakati au kukiuka mikataba ya mikopo, wananchi wanakimbilia kwenye mabaraza kwa kushauriwa na mawakili’’. Alisema Dkt. Mabula

Kwa mujibu wa Dkt. Mabula, ucheleweshaji mashauri kwa sababu zozote zile ni kuchelewesha kupata haki kwa wakati na kutoa rai kwa mawakili kuona umuhimu wa kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kutumia nafasi zao kama Maafisa wa Mahakama kwa nia ya kuhakikisha mashauri ya ardhi yanamalizika kwa wakati na kwa haki kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Allan Kijazi alisema, wizara yake imeitisha kikao cha pamoja na mawakili wa kujitegemea kwa lengo la kuhakikisha mashauri ya ardhi katika mabaraza yanasikilizwa na kumalizwa kwa wakati.

‘’Mawakili wa kujitegemea mnapotekeleza kwa uadilifu, uaminifu na weledi jukumu lenu la kuwakilisha wananchi katika mashauri mnawarahisishia Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi kazi ya kusikiliza na kutoa maamuzi kwa wakati kwani uwakilishi wenu kwa namna moja ama nyingine unatoa dira mapema ya kufahamu mwananchi yupi ana haki na yupi hana haki katika shauri husika’’ alisema Dkt. Kijazi.

Kikao Kazi cha Kitengo cha Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kina lengo la kupata uelewa wa pamoja, kupokea changamoto wanazokutana nazo katika mabarza ya ardhi pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya Wizara na TLS katika kutatua kero za wananchi nwenye mashauri ya ardhi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi