Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo leo Julai 30, 2022 ameshiriki katika zoezi la usafi wa mwisho wa mwezi katika Soko la Bonanza Jijini Dodoma.
Akiwa sokoni hapo amezungumza na wafanyabiashara na kutoa rai kwao kudumisha kwa vitendo kampeni ya usafi na mazingira kwa ujumla.
“Ndugu zangu agenda ya mazingira ni endelevu, sote yatupasa kuitekeleza kwa vitendo na uwe ni utamaduni wetu sote”, Dkt. Jafo alisisitiza.
Pia, amewapongeza wafanyabiashara sokoni hapo, mabalozi wa mazingira na wananchi kwa ujumla kwa kujitokeza kushiriki kufanya usafi wa mazingira
Amemwelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) ndani ya kipindi cha siku 14 kuhakikisha anafanya ukarabati wa mfumo wa maji taka katika soko hilo ili kuondoa adha inayowakumba wafanyabiashara kwa sasa.
“Ukarabati huu wa Mfumo wa maji taka katika eneo hili ufanyike mara moja, Mkurugenzi wa DUWASA asimamie kwa karibu utekelezaji wake”, Alisisitiza Dkt. Jafo.
Aidha, Waziri Jafo alisema kuwa Serikali inatarajia kuzindua Kampeni ya usafi wa mazingiraitakayofahamika kama ‘My Dustbin’ kwenye mitaa ya mbalimbali nchi nzima.
Alisema kampeni hiyo itasaidia kuweka mitaa katika hali ya usafi kwa kuwa kila mwananchi anatakiwa kutupa taka kwenye mapipa yaliyopo kwenye mitaa badala ya kutupa ovyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Mazingira na Udhibiti wa Taka ngumu wa Jiji la Dodoma, Bw. Dickson Kimaro alisema wamekuwa wakihamasisha wananchi kushiriki usafi wa mazingira ili kuweka jiji katika hali ya usafi. Bw Kimaro alilisitiza uwajibikaji wa kila mwananchi katika kuhakikisha usafi unafanyika mita tano kuzunguka maeneo ya Makazi na Biashara.
Alisema katika soko hilo wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla wamekuwa wakijitokeza kushiriki katika kufanya usafi wa mazingira sokoni hapo, hivyo kuliweka jiji katika hali ya usafi.