Na Shamimu Nyaki - WHUSM
Sekta za Wizara ya Habari ni sekta muhimu zenye mchango mkubwa katika kuchangia uchumi wa nchi na kuleta maendeleo.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dodoma na Waziri wa Habari , Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa wakati akiwasilisha Muundo pamoja na Majukumu ya Wizara hiyo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.
Mhe. Bashungwa amesema kwamba Sekta ya Sanaa na Michezo zimechangia katika Ongezeko la pato la Taifa ambapo kwa mwaka 2018, shughuli za burudani zimechangia pato la Taifa kwa asilimia 13.7 na kushika nafasi ya kwanza na mwaka 2019 shughuli hizo zilichangia asilimia 11.2 na kushika nafasi ya tatu.
"Tunashukuru Kamati kwa kutupa mawazo chanya ambayo yatasaidia kuboresha na kuendeleza sekta hizi, naahidi mimi pamoja na timu yangu tutayafanyia kazi mawazo mliyotupa na tayari tumeanza kufanya hivyo katika sekta zote" alisema Mhe. Bashungwa.
Akiendelea kuzungumza Mhe. Bashungwa ameeleza kuwa Wizara tayari imeanza kutengeneza Mpango Mkakati wa Maendeleo ya Michezo pamoja na ujenzi wa Ukumbi wa Michezo na Sanaa (Sports and Arts Arena) ambayo itaanza kujengwa Jijini Dodoma.
Aidha, Mhe. Bashungwa ameeleza kuwa TCRA pamoja na TRA wameanza kushirikiana namna ya kukusanya mapato ya kazi za Sanaa kupitia njia za Kidijiti (Digital Taxation).
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Stasilaus Nyongo Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki ameipongeza Wizara hiyo kwa Mikakati mizuri ya kusaidia Sekta inazozisimia, huku akishauri Wizara hiyo kuongeza ubunifu katika kukusanya mapato ya Serikali kupitia Sanaa na Michezo.
"Nashauri Wizara hii, Wizara ya Elimu pamoja na TAMISEMI kuwa na utaratibu unaotambulika wa kuendesha na kusimamia shughuli za michezo shuleni" Mhe. Nyongo.
Naye Mhe. Jumanne Sagini Mbunge wa Jimbo la Butiama ambaye ni Mjumbe wa Kamati hiyo amepongeza juhudi za Wizara hiyo katika kutekeleza majukumu yake ambapo ameeleza kuwa ipo haja ya kufanya mapitio ya Sera zote zilizochini ya Wizara hiyo ili kama kuna ambazo zinahitaji marekebisho zifanyiwe maboresho ili kuendana na mahitaji ya wakati huu.
Kamati hiyo imepokea taarifa ya Muundo na Majukumu ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo kesho Januari 26, 2021 itapokea Taarifa ya Majukumu ya Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo.