Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kuwahamasisha Wawekezaji kuwekeza katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori na misitu nchini hasa katika ujenzi wa huduma za malazi kwa ajili ya mahitaji ya watalii.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu vipaumbele vya mpango na bajeti ya mwaka 2022/2023 na jinsi vitakavyowanufaisha wananchi.
“Wizara ina mpango mahususi wa uwekezaji katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori na misitu ambapo sasa tuna orodha ya maeneo hayo chini ya taasisi za TAWA, TANAPA, TFS na Ngorongoro yakiwemo ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Mto Wami, Kizorobi, Kambi ya Masasi, Kisiwa cha Saadan, Mabata Makali, Mchondo, Uvinje, Chorangwa na Mkima. Kwa wale wanaohitaji kuwekeza wafike katika ofisi zetu kupata maeneo hayo”, alisema Waziri Pindi Chana.
Balozi Pindi Chana amefafanua kuwa, maeneo ya malazi yatakapoongezeka ni lazima miundombinu katika maeneo hayo iboreshwe ili shughuli za utalii ziweze kufanyika kwa wakati wote ikiwemo ujenzi na wa barabara mpya zenye urefu wa Km 2,500 katika Hifadhi za Taifa, kukarabati barabara zenye urefu wa Km 6,500, kujenga barabara za kutembea kwa miguu zenye urefu wa Km 342, kujenga vituo vitano vya kutua ndege katika mlima Kilimanjaro kwa ajili ya huduma za dharula na uokoaji, kukarabati viwanja vya ndege 17 na kutenga maeneo mapya 58 kwa ajili ya kujenga kambi za kitalii na nyumba za malazi.
Aidha, katika bajeti ya mwaka 2022/2023 Wizara imepanga kuboresha mifumo ya mawasiliano katika maeneo ya hifadhi ili kupata mawasiliano ya uhakika.
Aliyataja maeneo ya vipaumbele vya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kuwa ni kuendelea kutoa elimu juu ya mbinu za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu na kutoa elimu na mbinu rafiki kwa wananchi kudhibiti wanyamapori hao, kuendeleza programu ya The Royal Tour kwa kuongeza kasi ya utangazaji utalii kitaifa na kimataifa na kuibua masoko mapya ya utalii pamoja na kukarabati na kuimarisha miundombinu katika maeneo ya hifadhi.
Vipaumbele vingine ni kuibua na kuendeleza mazao ya utalii ya kimkakati ikiwemo utalii wa fukwe, mikutano na matukio, meli za kitalii, michezo na utamaduni, kuimarisha shughuli za upandaji miti, mazao ya Misitu na ufugaji nyuki na mnyororo wa thamani wa mazao hayo, Kuimarisha mfumo wa utoaji huduma za utalii ili kukidhi viwango vya kimataifa na kuboresha ulinzi na usalama wa rasilimali za maliasili na malikale.