Na Happiness Shayo - WMU
Wawekezaji wa sekta ya utalii kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni, wanatarajiwa kukutana jijini Arusha katika Mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) Kamisheni ya Afrika unaotarajiwa kufanyika Oktoba 5-7, 2022 jijini Arusha.
Maandalizi ya mkutano huo wenye kauli mbiu inayosema “Kuujenga Upya Utalii Stahimilivu wa Afrika kwa Maendeleo Jumuishi ya Kiuchumi na Kijamii” yanafanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza leo katika kikao cha tatu cha kamati ya kitaifa ya maandalizi ya mkutano huo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja amesema maandalizi yanaendelea vizuri huku akiwaelekeza wajumbe wa kamati hiyo kuendelea kufanya kazi vizuri ili kufanikisha mkutano huo kwa viwango vya juu.
“Ninaamini timu hii ni timu iliyokamilika, hivyo kila mjumbe atumie uwezo wake kufanya kazi vizuri ili tusimuangushe Mheshimiwa Rais,” Mhe.Masanja amesisitiza.
Naye, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Ndg. Juma Mkomi amesema Wizara itatoa ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha mkutano huo na pia kutatua changamoto zitakazojitokeza.
Mbali na wawekezaji, mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa UNWTO Ndg. Zurab Pololikashvili, Waziri wa Utalii wa Ivory Coast Ndg. Siandou Fofana na Mawaziri wa utalii kutoka nchi wanachama wa UNWTO.
Kwa mujibu wa aya ya 67 ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025, Serikali iliyopo madarakani inaendelea kuweka mkazo katika kupanua wigo wa bidhaa za utalii ili sekta hiyo iendelee kuchangia katika pato la Taifa.