Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Watumishi Wakumbushwa Umuhimu wa Kuishauri Menejimenti
May 18, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Jacquiline Mrisho.

Watumishi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wamekumbushwa umuhimu wa kuishauri Mamlaka yao ili iweze kufanya vizuri zaidi katika shughuli zake.

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Mohammad Kambi ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka hiyo.

Prof. Kambi amesema kuwa kikao hicho kinatoa fursa kwa watumishi kujadiliana juu ya masuala mbalimbali ya msingi yanayohusu tija na ufanisi wa mamlaka pamoja na maslahi ya watumishi wenyewe.

“Vikao hivi vinaonesha bayana namna ambavyo menejimenti inatambua umuhimu wa watumishi kushirikishwa katika maamuzi yanayohusu mamlaka hii, utaratibu huu ni mzuri kwani unaimarisha ushiriki wa wafanyakazi katika uendeshaji wa shughuli za mamlaka,” alisema Prof. Kambi.

Prof. Kambi amewasisitiza watumishi hao kuwa mikutano hiyo itumike kujadili malengo na mipango ya mamlaka na kushauri juu ya kuboresha utendaji ulio bora zaidi kwa sababu ni lazima tija na maslahi viwe na uwiano ili kuwa na matokeo ya utendaji kazi bora unaolenga kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi wanaowatumikia.

Amefafanua kuwa baraza la wafanyakazi mahali pa kazi lina wajibu mkubwa wa kuhakikisha kunakuwepo na maelewano, ushirikiano na mshikamano kati ya wafanyakazi na uongozi wa mamlaka vilevile baraza linatakiwa kuhakikisha kuwepo kwa nidhamu ya kazi kwa madhumuni ya kuleta tija ya ufanisi katika uendeshaji wa shughuli za mamlaka.

Aidha, ameeleza kuwa mchango wa mamlaka katika kutekeleza Sera  ya Wizara husika unadhihirika kutokana na uwajibikaji katika utekelezaji wa shughuli za kisheria na uchunguzi wa kimaabara kwa kutoa matokeo yanayosaidia mamlaka nyingine za kisheria kuweza kutoa maamuzi kwa wakati na yenye haki na hivyo kuleta utengamano katika jamii.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa GCLA , Dkt. Fidelice Mafumiko amesema kuwa katika uendeshaji wa shughuli za baraza kumekuwa na majadiliano chanya ambapo mwisho wa kikao yanapatikana maazimio safi yanayochukuliwa na kufanyiwa kazi na menejimenti.

Ameyataja baadhi ya masuala yatakoyojadiliwa yakiwemo ya hoja mbalimbali za TUGHE, kujadili na kupitisha bajeti ya mwaka 2018/19, kujadili na kupitisha taarifa ya utekelezaji wa nusu mwaka ya mwaka 2017/18 pamoja na kujadili na kupitisha muhtasari wa kikao kilichopita pamoja na yatokanayo na kikao hicho.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi