Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Watumishi wa Ardhi Watakaomilikisha Viwanja Mara Mbili Waonywa
Jul 08, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Na Munir Shemweta, WANMM

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema watumishi wa sekta ya ardhi watakaohusika kwa namna moja ama nyingine kumilikisha kiwanja kimoja mara mbili (Double allocation) watachukuliwa hatua kali.

Akizungumza mara baada ya kukagua shughuli za utendaji wa sekta ya ardhi kwenye banda la Wizara ya Ardhi katika maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba 7 Julai 7, 2021 alisema, ikibainika kuna umilikishaji wa ardhi mara mbili (Double allocation) uliosababishwa na watumishi basi wote waliohusika watachukuliwa hatua.

Alisema, awali sekta ya ardhi ilikuwa na migogoro mingi lakini tangu mwaka 2015 kero nyingi za sekta hiyo zimepungua kwa kiasi kikubwa.

"Ni kweli huko nyuma tulikuwa na kero nyingi sana katika sekta ya ardhi na nina amini tangu mwaka 2015 migogoro hakuna ama imepungua sana na nisisitize kama kuna utoaji hati mara mbili wote walioshiriki kuanzia wale wa kupima, kupanga na yule aliyemilikisha watachukuliwa hatua", alisema Lukuvi.

Kwa mujibu wa Lukuvi, Makamishna wa Ardhi Wasaidizi kwenye ofisi za ardhi za mikoa wanatakiwa kuhakikisha hakuna mgogoro mipya kwenye maeneo yao na kusisitiza kuwa ni marufuku ofisi hizo kushiriki ama kuchangia mgogoro wa ardhi.

Hata hivyo, Waziri wa Ardhi alibainisha kuwa kwa sasa Wizara yake imeanza kubadilika ambapo uandaaji na utoaji hatimiliki za ardhi umetoka kwenye mfumo wa analogia kwenda digitali na kusisitiza kuwa hayo ni mageuzi makubwa.

Akielezea zaidi mfumo wa kidigitali , Waziri Lukuvi ambaye pia alikabidhi hati za kielektroniki za papo kwa hapo kwa baadhi ya wananchi waliotembea banda la Wizara alisema  mfumo huo umeasisiwa na vijana wazalendo wa  kitanzania na lengo lake ni kuzuia makosa ya kibinadamu na kuongeza kuwa, anaamini migogoro inayosababishwa na tamaa za kibinadamu za watumishi itapungua.

Waziri wa Ardhi pia alitembelea Banda la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na kusifu ubunifu wa shirika hilo katika ujenzi wa nyumba za kuuza na kupangisha mkoani Dodoma katika maeneo ya Iyumbu na Chamwino.

Hata hivyo, alilitaka Shirika la Nyumba la Taifa kuhakikisha wananchi wanaolipa fedha kwa ajili ya kununua nyumba wanapatiwa nyumba hizo na kumilikishwa mara tu baada ya kulipa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi