Na.Mwandishi wetu - Morogoro.
Watumishi wa Serikali katika Sekta ya Afya, wametakiwa kuwa wazalendo katika kusimamia fedha za umma ili lengo la kufikisha huduma bora, kwa ukaribu na kwa wakati kwa wananchi litimie kama ilivyo adhma ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Wito huo umetolewa leo na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bw. Clifford Tandari alipokuwa akifungua mafunzo ya ugatuaji wa mipango ya afya na bajeti kwa utaratibu wa kupeleka fedha moja kwa moja kwenye vituo vya kutolea huduma (DHFF), kwa wadau wa afya kutoka Mikoa ya Arusha, Singida, Morogoro, Dodoma, Tanga, Kilimanjaro na Manyara.
‘’Suala la uwajibikaji katika Serikali ya Awamu ya Tano halina mjadala, mheshimiwa Rais alipoona mambo hayaendi sawa na kuna mkwamo mahala fulani akaamua kutoa maelekezo ya kupeleka fedha moja kwa moja kwenye vituo vya kutolea huduma, sasa nyinyi kama wasimamizi wa mchakato huo ni vema mkafanya kila liwezekanalo kuona ni jinsi gani mnasimamia fedha zinazotolewa na serikali na wafadhili ili zitumike tu kwa lengo lililokusudiwa tu” Alisema Bw.Tandari.
Alisema kipindi cha kufanya kazi kwa mazoea sasa kimekwisha na badala yake watumishi wajipange kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano, akitolea mfano falsafa ya wajapani ya ‘mutos spirit’ yaani kuongeza uwajibikaji na kufanya kazi za umma kama za kwako binafsi ili kuongeza ufanisi na matokeo chanya katika kila kazi inayofanyika.
“Mheshimiwa Rais anaongoza kwa mutos spirit ndio maana anafanyakazi kwa bidii na maarifa bila kuchoka wala bila kuwa na mawazo ya kwamba atashindwa hii na sisi watendaji tulio chini yake tuige, kwani wenzetu wameweza wana nini? Tujitahidi ndugu zangu kufanya kazi kwa kujituma na kwa uadilifu mkubwa ili basi na sisi baada ya muda mfupi tuonekane kuwa taifa lenye watu wachapakazi lakini pia wenye maendeleo’’ Alisisitiza.
Mpango wa ugatuaji wa madaraka ya uendeshaji wa huduma za afya katika ngazi za vituo unalenga kupunguza urasimu na kuboresha utoaji huduma za afya, ili kuimarisha utoaji wa huduma za afya, utaratibu wa kutoa fedha hasa mfuko wa Afya wa pamoja (Health Basket Fund) na mfuko wa malipo kwa ufanisi (Result based Financing) unaozingatia viashiria vya ufanisi vinavyopimika.
Kwa upande wake Dkt.Gemini Mtei ,Mkuu wa timu ya Mifumo ya Fedha kutoka Mradi wa uimarishaji mifumo ya Sekta za umma (PS3,Public Sector System strenghterning), amesema mradi huo umesaidia kujenga uwezo wa serikali katika utekelezwaji wa mpango wa DHFF,CHF iliyoboreshwa pamoja na PV.
Dkt.Mtei alisema PS3 kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto wamefanikiwa kufunga mifumo ya Mipango,Bajeti na utoaji taarifa ambayo imewezesha huduma kuwafikia wananchi kwa wakati na pia kwa urahisi kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Mradi wa PS3 unafadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia shirika lake la kimataifa la maendeleo la USAID, yenye lengo la kuisaidia serikali kutekeleza miradi ya koboresha sekta ya Afya na sekta nyinginezo kulingana na mahitaji na vipaumbele vya serikali.