Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), CPA Hosea Kashimba amezindua Maadhimisho ya Wiki ya Kimataifa ya Huduma kwa Wateja wa Mfuko huo leo Oktoba 5, 2023 Jijini Dodoma na kuwapongeza Watumishi wa Mfuko huo kwa utoaji wa huduma bora kwa wateja.
Akizindua maadhimisho hayo, CPA Kashimba ametoa huduma kwa wateja wa Mfuko huo na kuwapatia zawadi ikiwemo miche ya matunda ikiwa ni sehemu ya kampeni iliyozinduliwa hivi karibuni na PSSSF yenye lengo la kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
Akiongea wakati wa uzinduzi huo, CPA Kashimba amewashukuru watumishi wa PSSSF kwa kufanya kazi kwa bidii, kuimarisha ushirikiano baina yao ambao umechochea kutoa huduma bora na ubunifu wao uliosaidia mabadiliko makubwa kwenye huduma.
CPA Kashimba ametoa hamasa kwa watumishi kuendelea kujituma na ameahidi kutoa motisha kwa watumishi watakaojiongeza na kutoa ushirikiano mzuri.
Maadhimisho ya Kimataifa mwaka huu yana kaulimbiu isemayo "Team Service"; inayohimiza ushirikiano wa watendaji wote kwenye utoaji wa huduma maridhawa.
PSSSF inaadhimisha wiki ya Huduma kwa Wateja kwenye Ofisi zake nchi nzima, ambapo imeandaa programu mbalimbali za kuelimisha wanachama kuhusu huduma zake.
Maadhimisho ya Wiki ya Kimataifa ya Huduma kwa Wateja yanaadhimishwa duniani kote kila wiki ya kwanza ya mwezi Oktoba kuunga mkono juhudi za watoa huduma katika kutoa huduma bora.