Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Watu 3,500 Kunufaika na Mradi wa Maji Kalaela Wilaya ya Kalambo
Sep 20, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na. OMM Rukwa


Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingia Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Rukwa imefanikisha upatikanaji wa majisafi na salama karibu na wananchi kufuatia kukamilika kwa mradi maji wa kijiji cha Kalaela Wilaya ya Kalambo utakaohudumia wakazi 3,588.

Akizungumza kwenye hafla ya uwekaji jiwe la msingi la mradi leo (20.09.2022), Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Sahili Geraruma aliwapongeza RUWASA kwa kujenga mradi huo kwa ubora na kuwataka wahakikishe miundombinu iliyojengwa inakuwa imara na kuepusha maji kuvuja.

"Kila tone la maji ni dhahabu, hivyo watalaam pamoja na Mkandarasi fanyeni jitihada ili eneo lote la mradi wananchi sasa wapate huduma ya maji katika nyumba zao" alisema Geraruma.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kalambo, Mhandisi Patrick Ndimbo alisema jumla ya Shilingi milioni 152.5 kati ya Shilingi milioni 436.5 zimetumika kujenga mradi unaotekelezwa kupitia fedha za Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.

Mhandisi Ndimbo alieleza kuwa tayari mradi ulianza Februari mwaka huu na umefikia asilimia 90 na huduma ya maji imeanza kupatikana kwa wananchi wa kijiji cha Kalaela na utakamilika mwezi Octoba, 2022.

Alitaja kazi zilizokamilika kuwa ni ujenzi wa bomba kuu umbali wa mita 600, ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji lita 150,000, ujenzi wa bomba la kusambazia maji umbali wa mita 3,400 na ujenzi wa vituo nane vya kuchotea maji.

Katika hatua nyingine, Mwenge wa Uhuru umezindua mradi wa ujenzi vyumba vinne vya madarasa katika shule ya sekondari Mwazye uliogharimu Shilingi milioni Themanini ( 80,000,000).

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Tano Mwera alisema Mwenge wa Uhuru utakimbizwa na kupitia miradi mitano kwa kuweka mawe ya msingi, kuzindua na kukagua ikiwa na thamani ya Shilingi bilioni Moja na Milioni Themanini na Sita (1,086,800,000.0)

Kesho Jumatano, Mwenge wa Uhuru utaendelea na mbio zake katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbwanga.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi