Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Watanzania Watakiwa Kujenga Viwanda vya Kusindika Kahawa
Jul 13, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na. Frank Mvungi-Maelezo

Watanzania wametakiwa kujenga Viwanda vya kusindika Kahawa hapa nchini ili kuliiongezea thamani zao hilo hali itakayosidia katika kukuza  soko la ndani na kuzalisha ajira zaidi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya maonesho ya Kimataifa ya 41 ya Dar es Salaam (DITF), Afisa Masoko na Uhamasishaji wa Bodi ya Kahawa nchini Bw. Rogatus Meela amesema jukumu kubwa la Bodi hiyo ni kuhamasisha wananchi kutumia kahawa inayozalishwa hapa nchini.

Bw. Meela alikuwa akielezea wakati wa kuazimisha siku ya kahawa katika maonesho hayo ya yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu JK Nyerere Barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.

“Jukumu letu kubwa katika maadhimisho ya siku ya kahawa ni kuhamasisha watanzania kupenda kunywa kahawa inayozalishwa hapa nchini ambayo ina viwango vya Kimataifa kwa maana ya ubora na sisi kama wasimamizi tunaona kuna haja ya kuondoa kasumba iliyojengwa miongoni mwa Watanzania kupenda bidhaa za nje”, alisisitiza Meela.

Aliongeza kuwa kumekuwa na imani potofu kuwa Kahawa inaleta presha na magonjwa mengine kitu ambacho hakina ukweli kwa kuwa asilimia 90 ya kahawa ya Tanzania inauzwa katika mataifa yaliyoendelea ikiwemo Ujerumani, Italia, Japan na kwingineko duniani.

Kwa upande wake  Afisa Uhamasishaji wa  Bodi hiyo Bw. Frank Mlay  amesema kuwa swala la bei  ya kahawa linategemea soko la dunia ambapo Bodi hiyo imekuwa ikihakikisha kuwa wananchi wanapata bei bora kwa kuzingatia hali katika soko la dunia.

“Tunafanya kazi ya kuhakikisha kuwa tunasimamia zao la kahawa kuanzia shambani kwa kuhakikisha kuwa zao hili linachangia katika kujenga uchumi kama ilivyokuwa awali na wakulima wananufaika na hasa wanajitokeza kujenga viwanda vya kuongeza thamani hapa hapa nchini hali itakayosaidia kukuza sekta hii”, alisisitiza Mlay.

Bodi ya Kahawa Tanzania ni Taasisi ya Serikali yenye jukumu la kusimamia ustawi wa zao hilo hapa nchini na kuwasaidia wakulima kuongeza tija katika uzalishaji wa kahawa. Katika kutekleza jukumu hilo Bodi ilitenga siku maalum katika maonesho ya 41 ya Kimataifa ya Dar es Salaam ili kuhamasisha wananchi kunywa kahawa na kushiriki katika ujenzi wa viwanda vya Kahawa ili kuzalisha ajira.

   

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi