Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limetoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa za uwekezaji katika Hifadhi za Taifa ili waweze kunufaika na rasilimali hiyo inayovutia watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Akizungumza jana jioni katika kipindi cha Wekeza Tanzania kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Kaimu Kamishna wa uhifadhi TANAPA, Ndg. Juma Kuji amesema Tanzania ina jumla ya hifadhi 22 na kwamba shirika limebuni fursa mbalimbali za uwekezaji.
“Baadhi ya fursa hizo ni pamoja na uongozaji watalii wanaoruka kwa maputo (balloon safaris), ujenzi wa maeneo ya kulala wageni (hoteli na kambi za mahema), ujenzi na usimamizi wa kiwanja cha gofu, ujenzi wa viberenge (cable cars), ujenzi wa maeneo maalum ya uhifadhi (special tourism concession areas),” ameeleza Ndg. Kuji.
Pamoja na hilo, Ndg. Kuji amesema kwamba filamu ya Royal Tour imeongeza idadi ya watalii kutoka milioni 1.05 mwaka 2021/2022 hadi milioni 1.67 mwaka 2022/2023, hivyo kuongeza mapato kutoka shilingi milioni 174.7 kwa mwaka 2021/2022 hadi shilingi milioni 337.4 mwaka 2022/2023.
Sambamba na hayo, Ndg. Kuji amesema TANAPA imekarabati miundombinu na kutengeneza barabara ili watalii waweze kufika maeneo mbalimbali katika hifadhi lengo likiwa ni kuongeza idadi ya watalii hadi milioni tano ufikapo mwaka 2025.
Hifadhi za Taifa zilizopo nchini ni Arusha, Burigi-Chato, Gombe, Ibanda-Kyerwa, Katavi, Kigosi, Kilimanjaro, Kitulo, Ziwa Manyara, Mahale, Mikumi, Mkomazi, Nyerere, Ruaha, Rubondo, Rumanyika-Karagwe, Saadani, Kisiwa cha Saanane, Serengeti, Tarangire, Milima ya Udzungwa, na Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla.