Na. Frank Mvungi-Maelezo
Watanzania wameshauriwa kuwekeza katika ujenzi wa uchumi wa Viwanda vya nguo ili kukuza ajira na kupanua wigo wa uzalishaji bidhaa za ndani kulingana na mahitaji.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya Nguo, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji (Viwanda) Dkt. Adelhelm Meru amesema siku hiyo inaadhimishwa ikiwa ni sehemu ya maonesho ya 41 ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika viwanja vya J.K Nyerere, barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.
“Tayari Serikali imeanza Kuondoa changamoto zilizopo ikiwemo kutenga maeneo maalum kwa ajili ya ujenzi wa viwanda katika Mikoa yote hapa nchini, lengo likiwa ni kuvutia wawekezaji watakaojenga viwanda vya nguo”, alisisitiza Dkt. Meru.
Alieleza kuwa ili kuvutia uwekezaji katika sekta hiyo, tayari Serikali imetenga eneo maalum katika Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya nguo.
Katika kuhakikisha kuwa wataalamu wanaohitajika katika viwanda vya nguo wanazalishwa hapa nchini Dkt. Meru amesema kuwa kwa sasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeanza tena kuandaa wataalamu watakaotumika katika kukuza sekta ya nguo na hivyo baada ya muda changamoto ya wataalamu itakwisha kabisa.
Aidha, Dkt. Meru alindelea kuwasisitiza Watanzania Kuachana na Kasumba ya kupenda bidhaa za nje na badala yake wajenge utamaduni wa kutumia bidhaa za ndani zikiwemo nguo zinazozalishwa hapa nchini na viwanda vya Tanzania viweze kukua na kuchangia katika kuongeza ajira.
Aliongeza kuwa Serikali imeweka mkakati maalum wa kukuza sekta ya nguo hapa nchini kwa kuzitafutia ufumbuzi changamoto zote zinazokwamisha kukua kwa sekta hiyo likiwemo swala la mikopo kupitia Benki ya rasilimali Tanzania (TIB).
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tan Trade), ushiriki wa wazalishaji wa nguo umeongezeka mwaka huu kufikia 3,335 tofauti na maonesho ya mwaka jana ambapo washiriki katika sekta ya nguo walikuwa 2,500.