Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Watanzania wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutangaza matokeo ya Awali ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kwa kuwa yatasaidia kufahamu uhalisia wa ongezeko la watu nchini na namna ambavyo wanaweza kuletewa maendeleo.
Matokeo hayo ya awali yametangazwa leo jijini Dodoma na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Uwanja wa Jamhuri ambapo takwimu zimeonesha kuwa Tanzania ina jumla ya watu 61,741,120.
“Sensa ni kitu muhimu katika maisha, bila kujua idadi ya watu huwezi kufanya maendeleo yoyote, hivyo tunamshukuru Rais, Mhe. Samia kwa kutangaza matokeo haya, tunaamini nchi itafanya maendeleo zaidi kutokana na matokeo haya”, alisema Mwananchi wa Zanzibar, Bakari Kombo Omar.
Kwa upande wake, Profesa Miline Ngonile ameeleza kuwa matokeo haya ni matokeo sahihi kwa sababu yanakaribia kulingana na yaliyokuwa yanakadiriwa kabla ya Sensa pia yameweza kuonesha ongezeko halisi la watu waliopo Tanzania.
“Kwa kuwa Sensa ya Watu na Makazi imechukua takwimu hadi za kwenye Kitongoji basi mipango yetu ya maendeleo itafanyika kwa uhalisia kwani tayari tumeshafahamu uhitaji husika wa mahali fulani, sensa ina faida sana kwenye suala la maendeleo”, alisema Prof. Ngonile.
Bi. Hatia Juma kutoka Zanzibar amesema kuwa ni matarajio yake kwamba matokeo haya yatatumika katika kupanga taarifa za maendeleo zitakazotumika kupanga mahitaji ya watu kwa sababu ilikuwa haiwezekani kupanga chochote bila kuwa na takwimu.
Naye Bushishi Lema, mkazi wa Dodoma amepongeza jitihada za Serikali kwenye jambo hili na kusema kuwa kutangaziwa matokeo ni jambo zuri kwani ni haki ya kila Mtanzania kufahamu tuko wangapi ambapo matokeo hayo pia yatarahisisha uendeshaji wa shughuli za Serikali hasa utekelezaji wa wizara na taasisi za umma katika kuhudumia wananchi wake.