Watanzania wameaswa kuongeza juhudi katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zitakazouzwa nje ya nchi ili kukuza uchumi na kuongeza fedha za kigeni.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa wakati wa mkutano wake na waandishi jijini Dar es Salaam Agosti 26,2023 uliolenga kueleza utekelezaji wa Serikali na hutua zinazochukuliwa kutatua changamoto zinazojitokeza na kuathiri ustawi wa wananchi.
"Wizara zote zimetakiwa kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji kwenye sekta wanazosimamia ili kuendana na dhamira ya Serikali Kuhamasisha wananchi kuongeza uzalishaji", alisisitiza Msigwa
Akifafanua kuhusu dhana ya kuongeza uzalishaji,Msigwa amesema kuwa inamgusa kila Mtanzania ili kuendelea kujenga uchumi jumuishi na kuongeza kasi ya maendeleo.
Aidha, Msigwa ametoa wito kwa Wananchi kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa kuwabaini wale wote wanaojihusisha na biashara ya masoko ya fedha yasiyo rasmi (Black market) ili hatua za kisheria zichukuliwe na Serikali kwani biashara hiyo inaathiri uchumi.
Msemaji Mkuu wa Serikali amekuwa na utaratibu wa kueleza utekelezaji wa Serikali na hatua zinazochukuliwa katikati kuimarisha ustawi wa wananchi wote.