[caption id="attachment_40501" align="aligncenter" width="275"] Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchuni (NEEC) Bi Beng'i Issa.[/caption]
Na; Frank Mvungi
Serikali imesema kuwa itaendelea kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi mikubwa ili wachangie katika kujenga uchumi na kujiletea maendeleo kama ilivyodhamiria.
Akizungumza katika Kipindi cha “TUNATEKELEZA” Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi kiuchumi Bi Beng’i Issa amesema kuwa dhamira ya Serikali kupitia Baraza hilo ni kuwajengea uwezo wananchi ili waweze kushiriki kikamilifu katika miradi yote mikubwa inayotekelezwa hapa nchini.
“ Ajira zaidi ya asilimia 80 katika mradi wa ujenzi wa reli zimetolewa kwa watanzania na katika ujenzi wa bomba la mafuta na miradi yote mikubwa Serikali imeweka mkazo katika kuhakikisha kuwa ajira kwa kiwango kikubwa zinatolewa kwa watanzania,” alisisitiza Bi Beng’i
Akifafanua amesema kuwa sasa wananchi wana fursa ya kunufaika na miradi hiyo ikiwemo kutoa huduma mbalimbali katika miradi husika ambapo tayari Serikali inasimamia kwa karibu kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika kikamilifu kupitia hudumawatakazotoa katika miradi hiyo.
Akizungumzia uwezeshaji wananchi kupitia kituo kimoja cha uwezeshaji, Bi Beng’i amesema kuwa mpango wa Serikali ni kuhakikisha kuwa kuanza kwa kituo hicho katika Wilaya ya Kahama ni chachu ya kuanzishwa kwa vituo kama hivyo katika mikoa yote hapa nchini ili kusogeza zaidi huduma za uwezeshaji wananchi kiuchumi.Katika Vituo hivi taasisi zote zinazohusika na uwezeshaji wananchi kiuchumi zitakuwa katika eneo moja, akitaja taasisi hizo amesema kuwa ni pamoja na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) , MKURABITA, NSSF, SIDO, VETA, TBS,TRA, Mifuko ya Uwezeshaji wananchi kiuchumi, TASAF na Taasisi zote zenye jukumu la kuwasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi.
“Kituo cha Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Kahama kinahudumia wastani wa wananchi 100 kwa siku hali inayoonesha kuwa kuna uhitaji mkubwa wa kuwezesha wananchi kwa kuwajengea uwezo ili waweze kuzalisha kwa tija na kukuza uchumi,” alisisitiza Bi Beng’iAidha, Bi Beng’i amesema kuwa kuanzishwa kwa kituo kimoja cha huduma ni matokeo ya maagizo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa wakati alipotembelea Wilaya ya Kahama mwaka 2018.
Alibainisha kuwa Baraza hilo limeanzisha kanzi data ya wafanyabiashara ili kusaidia kuwaunganisha na fursa za miradi ya kimkakati inayotekelezwa hapa nchini ili iwanufaishe.
Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi limeanzishwa mwaka 2004 kwa lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi na limefanikiwa kuweka misingi madhubuti ya kuwakwamua wananchi kiuchumi.