Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Watafiti Watakiwa Kuisaidia Sekta ya Mifugo
Jul 22, 2022
Na Jacquiline Mrisho

 Na Mbaraka Kambona, Dodoma

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewataka Watafiti wa Mifugo nchini kuhakikisha wanafanya tafiti zitakazosaidia Sekta ya Mifugo kuzalisha kwa tija na kuwa na mchango mkubwa katika Pato la Taifa.

Waziri Ndaki alitoa wito huo wakati akifungua Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Mifugo uliofanyika jijini Dodoma Jana.

Akiongea na wadau hao, Waziri Ndaki alisema wafugaji wengi nchini bado wanafuga kienyeji  na kupelekea sekta ya mifugo kutokuwa na tija kubwa, hivyo ni wakati sasa watafiti wasaidie kutatua changamoto hiyo.

"Kama tutaendelea kufuga kama tunavyofuga leo kwa kuswaga Ng'ombe, baada ya miaka kumi ijayo tutaleta shida kwenye nchi hii, kwa sababu maeneo ya malisho yamepungua, hivyo watafiti watusaidie kuja na majibu yanayolenga kutatua changamoto hii, tuone namna gani tutakabiliana na jambo hili", alisema

Aliongeza kwa kusema kuwa kwa upande wa Wizara kuanzia mwaka huu wa fedha  wamejipanga kufanya kampeni kubwa ya kuwaelimisha wafugaji nchi nzima kuhusu ufugaji bora na wenye tija. 

"Tutaanza kutoa elimu  mwaka huu kuwaelimisha wafugaji kuhusu ufugaji bora na tutaendelea mpaka ujumbe huu wa kufuga kwa tija uwe umefika kwa wafugaji wote nchini", alifafanua

Aliendelea kusema kuwa Wizara imetenga bajeti kwa ajili ya kuelimisha wafugaji kuhusu malisho ya mifugo na mabadiliko ya tabianchi ili wabadilike kutoka kufuga kiasili na kufanya ufugaji wa kibiashara.

Kuhusu uhaba wa Wataalamu wa Ugani, Waziri Ndaki alisema mwaka huu Serikali itaajiri Maafisa Ugani zaidi ya 300 ili kupunguza changamoto hiyo huku akiongeza kuwa watanunua  pikipiki zaidi ya 1,000 kwa ajili ya kuwawezesha maafisa hao kuwahudumia wafugaji kwa urahisi.

Naye, Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Charles Mhina alisema kuwa maendeleo ya sekta ya mifugo kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na sekta binafsi hivyo Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wadau hao ili sekta hiyo iweze kuwa na mchango mkubwa katika Pato la Taifa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi