Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wapangaji Waiomba Serikali kuunda Mamlaka ya Udhibiti
Jul 20, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na. Paschal Dotto na Georgina Misama 

Chama Cha Wapangaji Tanzania (TTA) kimeiomba Serikali kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuunda Mamlaka Maalumu ya kudhibiti biashara ya kupangisha nyumba za makazi (Tenancy Regulatory Board).

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu wa TTA Bw. Ndumey Mukama alisema kwamba biashara ya kupangisha nyumba kwa ajili ya makazi imekuwa huria kiasi cha kila mmiliki wa nyumba kujipangia bei kulingana na matakwa yake.

“Kukiwa na Mamlaka maalum ya kushughulikia biashara ya upangishaji nyumba za makazi, kutaweka misingi ya haki na usawa kwa Watanzania katika matumizi ya nyumba kwa wapangaji”, alisema Mukama.

Akiongelea maslahi ya Taifa, Mwanasheria wa Chama cha Wapangaji Tanzania Bi. Pamela Kihumo alisema kwamba kuundwa kwa Mamlaka ya kudhibiti biashara ya wapangaji wa nyumba za makazi kutachochea kuongeza mapato kutokana na wamiliki wa nyumba hizo kulipa kodi kama wafanya biashara wengine.

Aidha, Pamela alisema kwamba, uwepo wa Mamlaka utaondoa malalamiko mengi ya utapeli kutoka kwa madalali ambao hujiweka katikati ya wapangaji na wamiliki wa nyumba kwa nia ya kujipatia pesa kwa kazi ya kumuunganisha mpangaji na mpangishaji.

Aliongeza kuwa Chama hicho kipo kuhakikisha kuwa raia wa Tanzania wa bila kujali umri, rangi na jinsia zote ambao ni wapangaji wa nyumba za makazi, biashara au mashamba wanalindwa wakiwa ni wateja wa huduma ya upangaji.

Alieleza kuwa TTA inapendekeza kuwa ni muhimu kuwa na Sera ya Nyumba (Housing policy), Sheria zaUupangaji (Tenancy Legislation) chini ya Mamlaka ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi ili kuweka mazingira safi kwa wapangaji.

Chama cha wapangaji Tanzania kilianzishwa mwaka 1985 kikiwa na dhamira ya kuweka mwongozo na mwelekeo wa kusaidia wananchi kupata makazi bora kwa wapangaji wote ndani ya Tanzania na kutoa huduma iliyobora katika mahusiano ya pande mbili yaani mpangaji na mpangishaji

Chama kina mahusiano mazuri na Serikali ya Jamhuri Muungano wa Tanzania kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) pamoja na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi na wanafanya kazi kwa pamoja katika kutambua uhitaji wa makazi kwa watanzania.

Aidha, TTA inatambulika kimataifa na kuiwakilisha Tanzania katika mahusiano ya karibu na vyama vingine Duniani kama Shirika la Makazi duniani (UN-Habitat) tawi la Tanzania, Vyama vya Wapangaji vya Afrika pamoja na Chama Kikuu cha Wapangaji Duniani (International Union of Tenants).

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi