Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wangabo Ataka Wafugaji Kupunguza Mifugo.
Nov 16, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_22695" align="aligncenter" width="750"] Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo  akiwatahadharisha wananchi kupunguza idadi ya mifugo ili kuhifadhi mazingira.[/caption]
Na.Mwandishi Wetu, Rukwa

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameiagiza kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya inayoongozwa na Mwenyekiti wake Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga kuhakikisha wanashirikiana na Halmashauri kupunguza idadi ya mifugo iliyopo kwenye halmashauri hiyo ili kudhibiti utunzaji wa vyanzo vya maji pamoja na hifadhi za misitu na kuliokoa ziwa Rukwa.

Amesema kuwa shughuli hizo za ufugaji karibu na vyanzo vya maji ndizo zinazosababisha kujaa kwa tope katika ziwa Rukwa, ziwa linaloasisi jina la Mkoa huo na kuongeza kuwa serikali haipo tayari kuona ziwa hilo likipotea na kusisitiza kuhifadhiwa kwa namna yoyote ile ikiwemo kupiga marufuku kufanbya shughuli za ufugaji kwenye vyanzo vya maji.

“Nashukuru kwamba zoezi la kupiga chapa linaendelea ila baada ya kumaliza zoezi hilo muanze kwenda boma kwa boma muhakikishe kwamba animal Unit “idadi ya mifugo kwa eneo” inazingatiwa, mtu ashauriwe kupunguza mifugo yake au ahame akatafute mahali pengine, kwasababu hatuwezi kujaza mifugo kwenye bonde la ziwa Rukwa halafu ziwa likafutika, serikali haitakubali.” alisisitiza.

  [caption id="attachment_22696" align="aligncenter" width="750"] Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara kijiji cha Kizumba Kata ya Laela Wilayani Sumbawanga.[/caption]

Mkuu huyo wa Mkoa alitoa maagizo hayo baada ya  kusomewa taarifa ya Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga katika Ziara yake ya siku mbili yenye lengo la kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo,pamoja na  kujitambulisha kwa watendaji wa serikali, watumishi pamoja  wananchi katika halmashauri hiyo.

Katika taarifa hiyo ilionesha kuwa idadi ya wanyama iliyopo katika bonde hilo ni 143,346 huku idadi inayotakiwa ni 36,666 huku ikionesha kuongezeka mara tatu zaidi ya mahitaji ya uwepo wa Wanyama hao katika bonde hilo.

Katika kulisisitiza hilo Mh. Wangabo amewatahadharisha wananchi kufuga kisasa kwa kuwa na mifugo michache yenye kuleta tija huku ikizingatia uhitaji wa ardhi kwaajili ya kilimo na shughuli nyingine za kibinaadamu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa skimu ya umwagiliaji Kijiji cha Ng’ongo, kata ya Mtowisa Wilayani Sumbawanga, Justin Amon amesema kuwa wafugaji wamekuwa wengi katika bonde hilo hasa katika skimu yao  na kuwasababishia hasara pale wanapopeleka mifugo yao kwaajili ya malisho.

“Kama taarifa ilivyosomwa wafugaji wapo wengi ambao wamegeuza eneo hili kuwa sehemu ya kuchungia, tunapojaribu kuwafuatilia wanatutishia  na mawe, fimbo, sime na mapanga na wapo tayari kupambana kwa lolote litakalotokea, na kesi zipo mahakamani lakini  tunaambiwa hatujakamilisha vigezo, hivyo tunashindwa kujua kwanini wanakingiwa kifua,” Alisema.

[caption id="attachment_22697" align="aligncenter" width="750"] Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiongea na wananchi wa Kijiji cha Zimba kwa lengo la kujitambulisha kwa wananchi hao wa bonde la ziwa Rukwa kata ya Mtowisa, Wilaya ya Sumbawanga.[/caption]

Wakati huohuo Mkuu huyo wa Mkoa wa Rukwa  amezitaka kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya kwa kushirikiana na watendaji wa kata na vijiji kuwakamata wazazi wa wanafunzi watoro ili kukomesha utoro mashuleni nahatimae kuongeza kasi ya ufaulu katika Mkoa.

Amesema kuwa haiwezekani wanafunzi wawe watoro na wazazi wapo hawafanyi lolote ili kuhakikisha watoto wao wanapata elimu stahiki kwaajili ya maendeleo yao, kuongeza ufaulu katika mkoa na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

“Nimesikitika kwamba matokeo ya shule yenu sio mazuri hayaridhishi, kuna utoro wa reja reja na utoro wa kudumu, nimeshaagiza hatua kali zichukuliwe dhidi ya watoro lakini kamati ya ulinzi na usalama muende mbali zaidi watoro wote wakamatwe hata wazazi pia wakamatwe, isiwe mtoto tu aliyetoroka, si ana wazazi wake, kamata mzazi mtoto peleka polisi wakajieleze vizuri,” Alisisitiza.

Aidha Mh. Wangabo amewasisitiza wanafunzi kuwa na maadili na nidhamu wawapo shuleni kwani kufanya hivyo kutawaongezea ufaulu na mafanikio katika maisha yao na kuongeza kuwa wanafunzi watukutu siku zote hawafanikiwi katika maisha na matokeo yake huishia mitaani.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi