Na Tiganya Vincent - RS TABORA
Wanavyuo Mkoani Tabora wameagizwa kuhakikisha kuwa wanatumia elimu wanayopata kuwa mabalozi watakaosaidia katika kuzuia uharibufu wa mazingira na kuwahimiza jamii kujenga utamaduni wa kupanda miti mipya na kulinda iliyopo kwa ajili ya manufaa yao ya sasa na baadae.
Kauli hiyo ilitolewa jana mjini hapa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati alipowaongoza wanavyuo kutoka Vyuo mbalimbali katika upandaji miti ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuhakikisha kila mtu anashiriki katika zoezi hilo.
Alisema kuwa wasomi kama wanavyuo wakiwa mstari wa mbele katika utoaji wa elimu katika maeneo yao yanayowazunguka na sehemu za baadae watakazopangiwa kazi ipo nafasi ya kuzuia uharibifu wa mazingira ikiwemo mistu kuendelea kuharibiwa.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa kitendo cha wanavyuo hao kuomba kuweka alama katika Mkoa wa Tabora kinapaswa kuwa mwanzo kwao katika katika kupeleka elimu hiyo katika maeneo mbalimbali ya jamii inayowazunguka ili wananchi wengi waweze kutambua umuhimu wa kutoharibu mazingira na vyanzo vya maji.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Tabora, Idd Moshi aliwataka Wanavyuo kuunga mkono juhudi za Mkuu huyo wa Mkoa kutaka kuigeuza Tabora kuwa ya kijana kwa kupanda miti ili kurudisha uoto wa asili.
Alisema kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora anafanya kazi nzuri ya kuhakikisha anasimamia agizo la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha mikoa yote hapa nchini inapanda miti mingi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Moshi alisema kuwa wanavyuo na jamii kwa ujumla wana jukumu la kuhakikisha kuwa wanawaunga mkono viongozi sio tu kwa kupanda katika maeneo ya umma pekee bali pia katika maeneo wanayoishi.
Alisema kuwa wao kama vijana wa CCM mkoa wa Tabora tayari wamepanda miti katika Wilaya za Igunga, Nzega, Sikonge na Urambo ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za viongozi wa Mkoa na Kitaifa.