Na Mwandishi Wetu-DODOMA
Wananchi Mkoani Dodoma wamepongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali katika Kujenga uchumi shirikishi unaogusa maisha ya wananchi baada ya Tanzania kutajwa na Jukwaa la Uchumi Duniani (World Economic Forum) kuwa nchi ya kwanza Kusini mwa Jangwa la Sahara kuwa na uchumi Jumuishi.
Akizungumza katika Mahojiano maalum mjini Dodoma Bibi Anyangwe Lupembe amesema ni jambo la kupongeza kwa hatua hiyo kwani haya ni matunda na juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kama ujenzi wa reli wa reli ya Kisasa (Standard Gauge) na Uzalishaji umeme.
Akifafanua Lupembe amesema kuwa kila mwananchi kwa sasa anaelewa kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuwahudumia wananchi wanyonge kwa kuhakikisha kuwa huduma muhimu zinapatikana kama Madawa, Elimu, miundo mbinu hali inayowapa fursa wananchi kushiriki katika shughuli za uchumi ikiwemo uzalishaji kutokana na mazingira wezeshi yaliyopo kwa sasa.
Aliongeza kuwa kasi ya ujenzi wa miundombinu kama barabara inawawezesha wananchi kushiriki katika uzalishaji na shughuli za maendeleo katika maeneo mbalimbali hapa nchi, hivyo uchumi kumilikiwa na wananchi.
Kwa upande wake Bwana George Nsavike amepongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kusimamia masuala ya Kodi ambayo ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ambapo kodi inayokusanywa inatumika katika kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo kwa sasa inawanufaisha wananchi wote hasa wa chini.
“Rais Magufuli ameonyesha mfano mzuri katika kusimamia rasilimali za Taifa yakiwemo madini na kusimamia ukusanyaji wa kodi ambapo wananchi wameonyesha kuunga mkono juhudi hizo ambazo zimechochea Kasi ya ukuaji wa uchumi” Alisisitiza Nsavike
Aliongeza kuwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano upelekaji wa umeme vijijini umepewa kipaumbele hali inayowapa wananchi fursa yakushiriki katika miradi ya maendeleo.
Naye Salmin Abdalah amesema ujenzi wa miundombinu na utekelezaji wa miradi mingine umewezesha wananchi kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijiletea maendeleo
Tanzania imetajwa na Jukwaa la Uchumi Duniani (World economic Forum) kuwa nchi yakwanza Kusini mwa janga la Sahara kwa kuwa na uchumi jumuishi hivi Karibuni.