Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wananchi 1700 Wamepata Huduma za Magonjwa ya Moyo Bila Malipo Kwenye Maonesho ya Saba Saba
Jul 12, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi Maalum

Wananchi 1776 wamepata  huduma za ushauri, vipimo na tiba za magonjwa ya moyo bila malipo zinazotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwenye maonesho ya 43 ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam yanayofanyika katika uwanja wa  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere uliopo barabara ya Kilwa.

Wananchi hao  waliotembelea banda la Taasisi hiyo  kwa ajili ya kupima afya zao walifanyiwa  vipimo vya magonjwa ya moyo ambapo  448 walifanyiwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi  (Echocardiography), na 1097 walifanyiwa kipimo cha kuangalia umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiogram - ECG).

Asilimia 60 ya watu waliofanyiwa vipimo walikutwa  na uzito mkubwa, asilimia 40 walikutwa na tatizo la  shinikizo la juu la damu na asilimia 20 walikutwa na tatizo  la kuwa na sukari kwenye damu.

Aidha Taasisi hiyo hadi sasa imetoa rufaa ya moja kwa moja kwa watu  73 wakiwemo watoto 2 ambao baada ya kuwafanyia vipimo walikutwa na matatizo ya moyo yanayohitaji kufanyiwa uchunguzi wa kina na matibabu ya kibingwa .

Akizungumzia mara baada ya kupata huduma ya matibabu katika banda hilo mkazi wa Shekilango jijini Dar es Salaam Rehema Abdalah aliipongeza Taasisi hiyo  kwa kutoa huduma ya matibabu ya moyo kwa wananchi bila malipo pamoja na kuwapa kipaumbele wazee waliojitokeza kwenda kupima afya zao.

“Nawashukuru wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete wanaotoa huduma katika maonesho haya, kutokana na umri wangu wamenipa kipaumbele cha kufanyiwa vipimo kwa haraka. Nimekutwa na tatizo la shinikizo la juu la damu na tayari nimepatiwa dawa kwa ajili ya matibabu,” alishukuru   Rehema.

Naye mkazi wa Mwananyamala jijini Dar es Salaam Hatibu Rashid ameishukuru Taasisi hiyo kwa kuwafikiria wananchi wenye uwezo wa chini kupata nafasi ya kufanyiwa vipimo vya magonjwa ya moyo na wafanyakazi wa Taasisi hiyo  pindi watakapopata nafasi watoe huduma kama hiyo  kwa wananchi waliopo maeneo mbalimbali hapa nchini hasa vijijini.

Rashid alisema, “Zamani vipimo kama hivi vilikuwa vinafanyika nje ya nchi tena kwa watu wenye hela. Lakini leo hii vipimo hivi vinafanyika hapa nchini na tunafanyiwa wananchi wa kawaida kabisa. Ninaishukuru sana Serikali kwa kuimarisha huduma ya matibabu ya moyo na ninawaomba wananchi wenzangu watumie maonesho haya kufika katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa ajili ya kupima afya zao bila malipo”,.

Katika maonesho hayo Taasisi hiyo inatoa bila malipo huduma za ushauri wa lishe bora kwa afya ya moyo, umuhimu wa kufanya mazoezi, vipimo na tiba za magonjwa ya moyo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi