Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wananchi 147 Waagwa Ngorongoro, Awamu ya Tisa
Sep 15, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mwandishi Wetu-MAELEZO

Serikali inaendelea na zoezi la kuhamisha wananchi kwa hiari katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro kuelekea kijiji cha Msomera mkoani Tanga.

Akizungunza wakati akiaga kundi la tisa lenye kaya 25 yenye wananchi 147 na mifugo 699, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro,
Raymond Mangwala amesema kuwa zoezi hilo linafuata haki zote za binadamu.

Zoezi hili linafuata haki za binadamu, wananchi wanazidi kuamasika kuhama kwa hiari, awamu hii ni ya tisa na wananchi wanahama kwa amani", amesisitiza Mhe. Mangwala.

Aidha, amesema kuwa, Serikali itaendelea kufanya maboresho ya zoezi hilo kadiri siku zinavyokwenda na uhitaji wake kwani maboresho ya kusajili wananchi kuanzia ngazi ya kitongoji, kijiji na hadi Kata imeleta mafanikio makubwa.

Hata hivyo Mhe. Mangwala ametoa wito kwa SUMA JKT kuendelea kujenga nyumba kwa kasi zaidi kwani muamko umekuwa mkubwa wananchi wanazidi kujiandikisha kuhama kwa hiari.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesisitiza kuwa Serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma bora popote walipo.

"Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inahakikisha wananchi wanapata huduma popote pale walipo, lakini katika eneo hili la Ngorongoro sheria ilikuwa inazuia baadhi ya vitu visifanyike kwa ajili yenu, kutokana na eneo mlilokuwepo, kama kujengewa shule, vituo vya afya na huduma nyingine", ameongeza Msigwa.

Nae Naibu Kamishna wa Uhifadhi Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dkt. Christopher Timbuka amesema kuwa baada ya kundi la tisa kuondoka itapelekea kaya 223 zenye wananchi 1,233 na mifugo 7,442 kuwa zimekwishahamia kiijiji cha Msomera mkoani Tanga.

Aidha, amesema kuwa,zoezi linazidi kuzingatia taratibu zote zinazotolewa na Serikali na kuhakikisha wananchi wanaohama katika eneo hilo wanapata stahiki zote.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi