Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wanachama wa SADC Waaswa Kupambana na Uhalifu
Jun 16, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Akida Abubakar – RS, MAMBO YA NDANI.

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Hassan Simba Yahya, amewaomba washiriki wa Mkutano wa Kamati Ndogo ya Usalama wa Raia ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kuhakikisha wanapambana kupunguza vitendo vya ujangili, biashara ya magendo, biashara ya binadamu na uhamiaji haramu

Alisema vitendo hivyo vinarudisha nyuma maendeleo ya nchi zilizopo katika Jumuiya hiyo, hivyo kupelekea kurudi nyuma kwa shughuli za maendeleo na uchumi.

Balozi Simba aliyasema hayo alipozungumza katika Mkutano huo   uliojadili masuala mbalimbali ya ulinzi na usalama katika maeneo ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo, uliohusu masuala ya uhamiaji, ukimbizi, mbuga na wanyamapori katika maeneo ya nchi wanachama wa jumuiya ya SADC, leo jijini Dar es Salaam.

“Hatuwezi kuendelea kiuchumi katika nchi zetu za wanachama wa   Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, kama matendo ya ujangili,biashara ya binadamu, masuala ya wakimbizi, uhamiaji haramu hayajatafutiwa ufumbuzi, kwani  haya yatazorotesha shughuli za kiuchumi ikiwepo utalii, hivyo ni bora tukayafanyia kazi maeneo hayo,” alisema Balozi Simba

Akizungumza wakati wa uchangiaji mada katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Masuala ya   Siasa, Ulinzi na Usalama wa   Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Jorge Cardoso, alisema uhalifu katika mipaka ya nchi wanachama ikiwemo uwindaji haramu wa pembe za ndovu, uhamiaji haramu,biashara ya binadamu na madawa ya kulevya lazima vidhibitiwe kwani vikiachwa mbeleni  vitahatarisha amani na utulivu uliopo katika nchi wanachama.

“Amani na utulivu katika nchi wanachama ni kichocheo cha mabadiliko ili kupiga hatua za kimaendeleo kwenda mbele na kushirikiana kukuza uchumi katika nchi wanachama wa SADC, hivyo yatupasa wote kwa pamoja kuunga mkono harakati za kukomesha vitendo vya uhalifu katika nchi na mipaka yetu,” alisema Cardoso

Washiriki wa mkutano huo kutoka katika nchi za Tanzania, Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Swaziland, Malawi, Zimbabwe kwa pamoja walikubaliana kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama katika nchi zao kudhibiti matendo yote yanayohatarisha amani na utulivu.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi