Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waliovamia Karantini ya Mifugo Watakiwa Kuondoka
Dec 24, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Na Mbaraka Kambona, Pwani

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka wananchi wakiwemo wafugaji waliovamia eneo la kuhifadhia na kuiangalia kwa muda mifugo  inayosafirishwa kwenda nje ya nchi kuondoka katika eneo hilo kwa hiyari huku akionya kuwa atakayekaidi Serikali itatumia nguvu kuwaondoa.

Waziri Ndaki alitoa wito huo alipotembelea eneo la Karantini ya Kwala iliyopo katika Wilaya ya Chalinze, mkoani Pwani Disemba 23, 2021.

Alisema kuwa eneo hilo lina maslahi mapana kitaifa na hivyo wananchi kuvamia na kufanya shughuli zao linafanya karantini hiyo kupoteza sifa ya kibiashara kimataifa.

"Hili eneo lina maslahi ya kitaifa hivyo wananchi walioingia na kukaa huku bila utaratibu wowote tuwaambie waondoke kwa hiyari, wale tutakaowakuta wakati tutakapoanza kazi ya ujenzi wa Karantini ya kisasa basi tutatumia nguvu kuwaondoa", alisema Mhe. Ndaki

Aidha, alisema kuwa mwaka wa fedha ujao watatenga fedha kwa ajili ya kuanza kujenga Karantini hiyo ili iwe ya kisasa itakayokidhi matakwa ya biashara ya kimataifa ya kusafirisha wanyama hai kwenda nje ya nchi.

"Hatuwezi kwenda kimataifa bila ya kuwa na kituo hiki, wenzetu wakija hapa ghafla na hali hii watatuambia msiuze Ng'ombe wala Nyama zenu kwa sababu hakuna mahali watakuwa wamehakikishwa kuwa  wako salama ", alifafanua

Awali, Mkuu wa Kituo hicho cha Kwala, Dkt. Othman Makusa alimueleza Waziri Ndaki kuwa kituo hicho kina miundombinu duni na kimevamiwa na Wananchi kutoka Vijiji vya jirani na wanafanya shughuli zao mbalimbali ikiwemo Kilimo, Makazi na Ufugaji jambo ambalo linasababisha kituo hicho kupoteza sifa za kimataifa za kuwa Karantini.

Katika hatua nyingine, Waziri Ndaki alisema kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wizara ya Nyumba na Maendeleo ya Makazi watakwenda kuliainisha eneo hilo vizuri na kuna baadhi ya maeneo ambayo wananchi wataambiwa wahame na maeneo mengine yatabakishwa kwa wananchi ili waendelee na shughuli zao.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi