Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waliopata Ujauzito Kufukuzwa Shule si Jambo Jipya -Majaliwa
Jul 05, 2017
Na Msemaji Mkuu

Asema ni utekelezaji wa Waraka na Kanuni za Elimu za mwaka 2002

                                                     WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema msimamo wa Serikali wa kutoruhusu wanafunzi waliopata ujauzito kuendelea na masomo katika mfumo rasmi wa elimu umetolewa kwa mujibu wa Sheria na sio utaratibu mpya kama inavyopotoshwa na baadhi ya wanaharakati.

Waziri Mkuu ametoa ufafanuzi huo leo (Jumatano, Julai 5, 2017) katika hotuba yake ya kuahirisha Mkutano wa Saba wa Bunge mjini Dodoma.

Amesema msimamo huo wa kisheria unalenga kuwafanya watoto wa kike wajishughulishe na masomo yao zaidi badala ya kushiriki kwenye vitendo vya ukiukwaji wa maadili.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2015, jumla ya wanafunzi 3,637 waliacha masomo kutokana na kupata ujauzito.

“Kuwaachisha masomo wanafunzi waliopata ujauzito ni utekelezaji wa Waraka na Kanuni za Elimu za mwaka 2002, zinazoruhusu kufukuza na kuondoa wanafunzi shuleni kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo uasherati, wizi, ulevi, kutumia dawa za kulevya pamoja na utoro.”

“Lengo hili lina nia ya kuwahimiza wazazi wawafundishe watoto wao mambo mema ndani ya familia na wawakataze kushiriki vitendo vya ngono katika umri dhamira ya Serikali ni kumlinda mtoto wa kike ili apate elimu kwa ajili ya manufaa yake na Taifa kwa ujumla.”

Waziri Mkuu amesema kila Mtanzania ana wajibu wa kuhakikisha kuwa watoto wote wanapata elimu. Hivyo ni lazima tuhakikishe mtoto wa kike anapata elimu stahiki na masomo yake hayakatizwi kwa kupata ujauzito.”

Amesema Serikali imewekeza kwenye mtoto wa kike, ambapo kifungu Na. 60 (b) cha Sheria ya Elimu Sura ya 353, kinatoa adhabu ya miaka 30 jela kwa yeyote atakayeoa au kumpa ujauzito mwanafunzi.

Pia, sheria inatoa adhabu ya kifungo cha miaka mitano jela au faini ya shilingi milioni tano, au vyote kwa pamoja kwa anayeshiriki kumuozesha mtoto wa shule. 

“Natoa wito kwa Wakuu wa Wilaya kusimamia utekelezaji wa Sheria za nchi zenye lengo la kumlinda mtoto wa kike. Aidha, nawashauri Waheshimiwa Wabunge, mshirikiane na Halmashauri zenu kuweka mikakati ya kudhibiti ujauzito kwa watoto wa shule.”

 Wahamasisheni wananchi watoe ushirikiano kwa vyombo vya dola, ili wanaowapa wanafunzi ujauzito au kuwakatisha masomo ili waozeshwe wapate adhabu stahiki.

 

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

S. L. P. 980,

40480 - DODOMA.        

JUMATANO, JULAI 05, 2017

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi