Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wakuu wa Mikoa Watakiwa Kufanya Uhakiki wa Takwimu za Operesheni Anwani za Makazi
May 24, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mwandishi Wetu, DODOMA

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amewataka Wakuu wa Mikoa yote 31 nchini kufanya uhakiki wa takwimu za operesheni ya Anwani za Makazi katika mikoa yao hasa katika kipengele cha usimikaji wa miundombinu ya nguzo zenye majina ya barabara na mitaa pamoja na namba za nyumba 

Akizungumza katika kikao kazi na Wakuu wa Mikoa kilichofanyika leo Mei 24, jijini Dodoma, Waziri Nape amesema kuwa uhakiki huo ni muhimu kwa kuwa takwimu za usimikaji wa miundombinu hiyo zinaonesha zipo chini ukilinganisha na uhalisia wa kilichotekelezeka katika mikoa ambayo kwa nyakati tofauti yeye binafsi pamoja na viongozi wengine walipita kukagua na kuridhika na utekelezaji

Ameongeza kuwa ifikapo siku ya Ijumaa Mei 27, Wizara hiyo itakuwa imepeleka fedha kwenye mikoa yote kwa ajili ya kufanya zoezi la uhakiki na kuweka takwimu sawa kulingana na uhalisia ili taarifa itakayowasilishwa ikiwa imesainiwa na Mkuu wa Mkoa husika iwe sahihi na ndio itakayokabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

“Ukiangalia hali ya takwimu kwa mfano Mkoa wa Lindi inaonekana ni asilimia mbili tu ya physical signs ndio imetekelezwa, lakini uhalisia haupo hivyo kwa kuwa nimepita mikoa mingi hadi Zanzibar nimejionea lakini bado takwimu zinaleta utata hivyo niwaombeni sana twendeni tukahakiki ili sisi na nyie tuzungumze lugha moja kwa kupata takwimu halisi”, Amezungumza Waziri huyo.

Waziri Nape amesema kuwa,” Zoezi hili la Anwani za Makazi limethibitisha uwepo wa Serikali za Mitaa zilizo imara na zinazomwakilisha vizuri Rais wetu na kama mtu ana mashaka na uimara wenu Wakuu wa Mikoa mie nitakuwa balozi wenu kwa sababu nimepita katika mikoa nimekagua na nimeridhika lakini pia ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Ardhi na TAMISEMI wamepita kukagua na wamejionea mmefanya kazi nzuri sana”.

Aidha, Waziri Nape ametumia kikao hicho kupenyeza ajenda ya Wizara anayoisimamia ya kuipeleka nchi katika uchumi wa kidijitali ambapo Wizara hiyo imejipanga kufanya semina kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala ili kuzungumzia uchumi wa kidijitali unaendaje, nini kinatakiwa kufanyika na maeneo wanayopaswa kushiriki 

Kwa Upande wa Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. David Silinde amewataka Wakuu wa Mikoa kusimamia Kanuni za utekelezaji wa Anwani za Makazi ambazo ndio msingi wa utekelezaji wa zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kuwabana watendaji kutumia fedha za mapato ya ndani bila kuathiri wala kutumia fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi mingine ya maendeleo

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa zoezi la utambuzi wa makazi ya watu ni moja ya eneo muhimu litakalosaidia nchi kuingia kwenye uchumi wa kidijitali ambao hauna mipaka na unaoruhusu wananchi kujihusisha na shughuli za kiuchumi mahali walipo

“Niwashukuru sana Wakuu wa Mikoa kwa kufanya kazi hii kwa kiwango cha juu na ufanisi mkubwa ambapo sasa tumefikia asilimia 106.62 ya utambuzi wa makazi ambapo asilimia hizi zimedhihirisha kuna makazi tuliyokuwa hatuyatambui awali na kupitia zoezi hili tumeyatambua na yatajumuishwa kwenye mipango ya maendeleo  

Amesema kuwa kuna mafanikio mengi yamepatikana kupitia mfumo huo ikiwa ni pamoja na mfumo wa utambuzi wa NaPA ambao ni endelevu na utasaidia nchi kuendelea kutambua na kuhifanyi anwani za makazi na kutimiza nia ya Wizara hiyo ya kuifanya nchi kuwa na uchumi wa kidijitali sambamba na huduma za TEHAMA kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, minara ya mawasiliano, ujuzi na matumizi ya mifumo pamoja na usalama wa mitandao 

Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Utawala, Kasper Mbuya, amewashukuru na kuwapongeza Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala na wataalamu kwa kazi nzuri ya kutekeleza maelekezo na maagizo yaliyotolewa na Rais na zoezi linalofuata la uhakiki ni kuboresha kwa ajili ya kupata takwimu halisi ya kilichotekelezwa

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Wakuu wa Mikoa, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack amesema kuwa wakuu hao ndio timu ya ushindi katika shughuli zote za Serikali zinazoelekezwa katika mikoa yote ya Tanzania bara na Zanzibar kinachotakiwa kufanyika ni kuboresha huduma za mawasiliano ya intaneti ili kusaidia kuboresha utekelezaji endelevu wa mfumo wa Anwani za Makazi nchini

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Clarence Ichwekeleza amesema utekelezaji wa mfumo wa Anwani za Makazi ni mfumo wa msingi utakaowezesha uchumi wa kidijitali na ulianza kutekelezwa mwaka 2010 na jitihada nyingi zimefanyika baada ya hapo lakini bado lengo halikutimia mpaka baada ya zoezi hilo kuwa operesheni maalumu utekelezaji umekuwa na mafanikio makubwa kwa muda mfupi

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi