Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wakulima wa Mpunga Katika Sikimu ya Ussoke Mlimani Wapewa Siku Sita Kukamilisha Mifereji ya Usambazaji Maji Mashambani Mwao.
Nov 13, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Tiganya Vincent, Rs –Tabora

WAKULIMA wa Mpunga katika Mradi wa Umwagiliaji wa Ussoke Mlimani na Yelayela ambao hadi hivi sasa hawajakamilisha uchimbaji wa mifereji inayosambaza maji kutoka mfereji mkuu kwenda kwenye mashamba yao wametakiwa kuhakikisha wamekamilisha zoezi ndani ya wiki hii.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni katika eneo la mradi lilipo Ussoke Mlimani na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo  Margaret Nakainga  wakati wa kikao kati ya Uongozi wake na Wakulima wanachama mradi huo wa umwagiliaji.

Alisema kuwa baada ya muda waliokubaliana katika kikao hicho kumalizika , watakaokuwa wameshindwa watachukuliwa hatua na viongozi wao kulingana na maamuzi waliofika ili wasiendelee kuwa kikwazo cha kutaka kurudisha nyuma ufanisi wa mradi huo uliotumia fedha nyingi.

Nakainga alisisitiza kuwa ucheleweshaji wowote unaweza kusababisha baadhi ya wakulima washindwe kulima kwa sababu ya mkulima aliyemtangulia hajachimba mfereji ambao utaruhusu maji yapite kwake kisha yaende kwa jirani yake.

“Natarajia kuja kukagua siku ya Ijumaa kama mtakuwa mmekamilisha kuchimba mifereji kama tulivyokubaliana katika kikao hiki, atakayekuwa hajakamilisha tutaona ni hatua gani tuchukue ili asije akawa kikwazo kwa wanamradi wengine” alisisitiza DED.

Naye Mwenyekiti wa Mradi huo, Bryson Kazala aliwataka wakulima ambao hawajakamilisha maandalizi ya mashamba yao kufanya hivyo mapema la sivyo watalazimika kuwanyang’ana na kuwagaiwa waliokuwa tayari kuyaendeleza.

Alisema kuwa ni lengo la mradi huo kutaka kila eneo lililopimwa lifanye kazi ya uzalishaji ili hatimaye waweze kuishawishi Serikali ipanue eneo la mradi kwa ajili ya kuingiza wanachama wengi zaidi.

Kazala alisema kuwa ni vema kila mkulima aliyeomba shamba na kupatiwa akahakikisha ndani ya muda waliojipangia anaweka eneo lake vizuri tayari kwa ajili ya kilimo hicho.

Kwa upande wa Katibu wa Mradi huo Rajab Karunguyeye alisema kuwa ikiwa wanachama waliojiandikisha katika mradi huo watawajibika ipasavyo wataondoa suala la kuagiza mchele kutoka nje ya kijiji na kuwa ziada ya kuwauzia watu wengine.

Mradi huo ambao umegharimu zaidi ya shilingi milioni 800 una mashamba ambayo yana ukubwa wa hekta 211 ambayo ni kwa ajili ya kilimo cha kisasa cha umwagiliaji mpunga.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Nakainga ametoa wito kwa Wakulima wote wilayani humo kutumia mvua zilizoanza kunyesha kulima mazao mchanganyiko kwa ajili ya chakula na biashara.

Alitaja baadhi ya mazao hayo kuwa ni mihogo, viazi vitamu, mahindi , alizeti , pamba, karanga na tumbaku kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wanakuwa na mazao ya aina mbalimbali ambayo yatakuwa chanzo cha chakula na wanaweza kuyauza kwa ajili ya uboreshaji wa maisha ya familia zao.

Nakainga aliwataka wanapolima wazingatie maoni ya wataalamu ili waweze kupata mazao bora na mengi.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi