Na. Paschal Dotto-MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amewataka watumiaji wa mitandao ya kijamii pamoja na Waandishi wa Habari Afrika kutumia taaluma zao kuandika habari kuhusu uzuri wa bara hilo pamoja na kuzingatia mila na desturi zake katika kazi zao za uandishi.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani leo Mei 3, 2022 ambayo kwa Afrika yamefanyika nchini Tanzania Jijini Arusha, Rais Samia amewataka waandishi wa Habari wa Afrika kuandika mazuri ya nchi zao ikiwemo utajiri wa rasilimali na uzuri wake pamoja na mila na desturi ili kulinda hadhi ya nchi zao.
“Mkikaa kimya hakuna atakayelisemea bara hili hivyo wakati wengine wakizungumza migogoro nyie zungumzieni amani, wakizungumza umasikini zungumzieni maendeleo pia waelimisheni wananchi kuacha mila potofu lakini pia kupitia kazi zenu za uandishi mna jukumu la kusaidia kukuza uchumi wa nchi zetu za Afrika”, Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amesema kuwa mitandao ya kijamii imekuwa ni sehemu muhimu ya maisha ya watu ambayo ni pamoja na Instagram, Twitter na Youtube. ambapo inatoa fursa ya kutumia Uhuru wa kujieleza, kukubaliana au kutokubaliana na masuala mbalimbali katika jamii.
"Sisi Waafrika tuna mila na desturi tunazotakiwa kuzitunza na kuziheshimu mengine yanayotokea mitandaoni na kwenye vyombo vya habari hayaangalii hayo, tunakopa kule, kule tunakokopa lililo sahihi kwao haliko sahihi kwetu lakini tunasahau hivyo vyombo vya habari visimame vyema kutekeleza katika kulinda mila na desturi zetu" Alisisitiza Rais Samia.
Rais Samia aliongeza kuwa uhuru vya Vyombo vya Habari ambao upo Tanzania kwa kiasi kikubwa unatokana na utashi wa kisiasa kwani wakati Tanzania inapata uhuru kulikuwa na magazeti 10 lakini sasa hivi kuna magazeti 285 na redio moja kwa sasa kuna zaidi ya redio 200, hakukuwa na kituo cha runinga lakini kwa sasa kuna vituo 55 vya runinga.
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amesema kuwa Serikali inaheshimu na kulinda uhuru wa vyombo vya habari nchini pamoja na uhuru wa kutoa mawazo kwani Serikali ya Awamu ya Sita imebadilisha mambo mengi kuinua tasnia ya habari.
“Kufanyika kwa maadhimisho haya ni matokeo ya kazi nzuri uliyofanya katika kipindi cha mwaka mmoja ulichokaa madarakani, ambapo umebadilisha mambo mbalimbali yaliyoleta sifa mpaka nje ya Tanzania, maadhimisho ya maonyesho haya yalianza Mei mosi, 2022 na kilele chake ni leo Mei 3, 2022, ambapo wanahabari kutoka nchi mbalimbali za Afrika wamekuwa na muda mzuri wa kujadili kwa kina na kujifunza pamoja na kubadilishana uzoefu katika mambo kadhaa kuhusu tasnia ya habari”, alisema Waziri Nape.
Waziri Nape amesema Wizara yake itahakikisha kuwa inaimarisha ushirikiano na vyombo vya habari na wadau wa habari hapa nchini na nje ya nchi pamoja na kusimamia maslahi ya wanahabari na kuifanya sekta hiyo kukua na kuwa na mchango mkubwa kwa taifa.
Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa atahakikisha anaifanya tasnia hiyo kuwa katika sehemu ambayo taifa litanufaika na sekta hiyo ili kuleta maendeleo kwa kila mwananchi.
“Sisi tuna makusudi na nia thabiti ya kutumika na kuitumikia Tanzania kwa kuifanya teknolojia ya habari na mawasiliano pamoja na sekta ya habari kuwa nguzo imara katika kuchochea uchumi wa Tanzania na wa Dunia kupitia Tanzania”, Alisema Dkt. Jim Yonazi.
Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari kidunia inaadhimishwa nchini Uruguay na kwa Afrika kwa mara ya kwanza inaadhimishwa katika Jiji la Arusha nchini Tanzania ambapo nchi 54 zimeshiriki katika mkutano huo.