Na Anthony Ishengoma - Dodoma
Wakazi takribani 150 wa Kata ya Mkonze Jijini Dodoma wamejitokeza mbele ya Kamati iliyoundwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Allan Kijazi iliyojikita Jijini Dodoma kuhakikisha inamaliza kero zote za ardhi ndani ya Jiji la Dodoma.
Wakazi hao wamejitokeza kwa makundi tofauti kutoka Mitaa ya Kata ya Mkonze ambapo zoezi limeanzia ili kuwasilisha malalamiko yao mbele ya kamati hiyo huku madai yao yakitofautiana kulingana na aina ya migogoro ambayo kila mwananchi anakabiliana nayo.
Akifafanua kuhusu aina ya malalamiko ambayo Kamati imeyabaini baada ya kukutana na Wananchi wa Kata hiyo, Kamishna wa Ardhi Nchini, Nathaniel Methew alisema mpaka sasa Kamati imebaini kuwa kuna migogoro ya muda mrefu ambayo ilianza tangu enzi za Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA), hivyo kutoa taswira tofauti ya namna migogoro hiyo ilivyojitokeza.
Kamishna Methew aliongeza kuwa, timu yake imebaini pia migogoro hiyo imechangiwa na baadhi ya taratibu za urasimishaji viwanja ambao haukuzingatia uwiano wa asilimia 30/70, hivyo baadhi ya wananchi kushindwa kupata asilimia zinazotakiwa jambo ambalo pia limezua mamalalamiko hivyo timu hiyo itaangazia namna bora ya kutatua kero hiyo.
Aidha, Kamishna ametaja chanzo kingine cha migogoro hiyo ikiwemo kuwepo kwa kundi kubwa la wananchi wa Kata ya Mkonze wanaolalamikia eneo la ukanda wa kijani uliopo eneo la Biawana na kusema kuwa Wizara itaweka utaratibu wa kuona namna bora ya kushughulikia mgogoro huo kwa wananchi wa eneo hilo.
Akiangazia zaidi kuhusu malalamiko hayo, Kamishna Methew alitaja uwepo wa changamoto ya umilikishaji viwanja mara mbili au kumili kiwanja kimoja kwa zaidi ya mtu mmoja jambo ambalo timu ya wataalam inalifanyia kazi ili kutoa haki kwa wakazi hao.
Mzee John Samwel Mlonganile, Mkazi wa Kata ya Mkonze aliviambia vyombo vya habari kuwa anaiomba Serikali kuingilia kati na kumaliza mgogoro wa Shamba lake ambalo anadai limemegwa na Shirika la Umeme TANESCO bila kumpa fidia akidai wamejaribu kuwasilisha malalamiko yake na wenzake 47 katika ngazi mbalimbali bila mafanikio.
Mzee Mlonganile amesema amemiliki shamba hilo toka Mwaka 1945 na tangu wakati huo ameishi hapo akifanya shughuli za kilimo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya maji, hivyo kuitaka Serikali kuingilia kati kumaliza mgogoro wao dhidi ya TANESCO.