Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wahitimu JKT Msange Watakiwa Kuwafichua Maadui wa Umoja wa Watanzania
Sep 16, 2017
Na Msemaji Mkuu

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri akihutubia jana mjini hapo katika sherehe za  kufunga mafunzo wa vijana  wa Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria ambayo yanajulikana kama Opereshi Tanzania ya Viwanda  katika Kikosi  cha Jeshi cha 823 JKT Msange jana wilayani Tabora.

Na: Tiganya Vincent - RS Tabora

 Wahitimu wa Mafunzo ya Mujibu wa Sheria Operesheni ya Tanzania ya Viwanda wametakiwa kutumia elimu waliyopata kuhakikisha kuwa wanakuwa wazalendo na watiifu kwa wananchi na Serikali yao ili kuhakikisha kuwa nchi hii haingiliwa na adaui yoyote kwa makusudi ya kuvuruga amani iliyopo.

 Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri jana wilayani Tabora wakati akifunga mafunzo wa vijana  wa Jeshi la Kujenga Taifa Opereshi Tanzania ya Viwanda  katika Kikosi  cha Jeshi cha 823 JKT Msange.

Aliwaeleza wahitimu hao kuwa ni vema wakatumia mafunzo waliopatiwa katika kuwafichua wale wote wenye nia mbaya ambao wanaishi katika jamii zao na wale wanaoingia nchi kwa njia za panya ambao wanakusudia kuendesha vitendo vinavyohatarisha umoja wa Watanzania.

Wahitimu wa Mafunzo ya Mujibu wa sheria  Opereshi Tanzania ya Viwanda wakila kiapo cha Utii wa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ambaye pia ni Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania katika sherehe zilizofanyika jana mjini Tabora katika Kikosi  cha Jeshi cha 823 JKT Msange.

 “Maadui wamebadili medani za kufanya uhalifu …ni vema mkatumia mafunzo hayo mliopatiwa na makamanda wetu kuwafichua watu wenye nia ovu ili hatua dhidi yao zichuliwe na Tanzania iendelee kuwa moja”, alisisitiza Mwenyekiti huyo wa Mkoa wa Kamati ya Ulinzi na Usalama.

 Aidha Mwanri aliwasisitiza Wahitimu hao kulinda viapo vyao kwa kuzingatia nidhamu na utiifu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Tanzania na Serikali yake na wananchi kwa kuwa makini kulinda nchi ili maadui wasiingie nchini na kuaharibu umoja wa Taifa.

Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa nchini (JKT) Brigedia Jenerali Elizaphania Marembo aliwashauri wahitimu wa mafunzo ya JKT kujiepusha na Wanaharakati watakapokuwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwani wapo ambao lengo lao ni kuhakikisha nchi inavurugika na Watanzania wanagawanyika.

Alisema kwa wale watakaobahati kujiunga na vyuo vikuu hapa nchini ni waende kuwa  mabalozi wazuri wa kuwaelimisha vijana ambao hawakupata fursa ya kujiunga na JKT kuacha migomo, kutojihusisha na matendo maovu kama vile matumizi ya dawa za kulevya na vinavyoweza kuwasababisha wapate magonjwa ambayo yanaweza kuchangia kupoteza ndoto zao.

Kwa upande wake Mkuu wa Bregedi ya 202 kundi la Vikosi vya Kanda ya Magharibi (FARU) Brigedia Jenerali Stephen Mkumbo aliwataka wahitimu hao kuwa mabalozi wa masuala ya ulinzi na usalama katika maeneo yao ili Tanzania iendelee kuwa kisiwa cha amani.

Alisema kuwa kuna baadhi ya vitendo vyenye viashiria vya ugaidi, hivyo ni vema wakatumia mafunzo waliopatiwa kuwa vyanzo vya taarifa ambazo ni hatarishi kwa usalama nchi ya Tanzania na Jeshi lake.

Mwakilishi wa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa chini (JKT) Brigedia Jenerali Elizaphania Marembo, akiwahutubia wahitimu wa mafunzo ya JKT Opereshi Tanzania ya Viwanda  kutoka kambi ya JKT Msange mkoani Tabora jana. Brigedia General Marembo aliwaasa wahitimu kujiepusha na Wanaharakati watakapokuwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwani wapo ambao lengo lao ni kuhakikisha nchi inavurugika na Watanzania wanagawanyika.

Mkuu wa Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa Msange  (823 KJ) Luteni Kanali Mohammed Mketto alisema kuwa vijana hao wa mujibu wa Sheria waliingia kambi hapo wakiwa 1,543 na wamefanikiwa kumaliza mafunzo yao wote.

Alisema kuwa miongoni mwao wamefanya usahili wa kujiunga na Jeshi la Wananchi wa Tanzania na hivyo wanasubiri majibu kuingia rasmi katika mafunzo zaidi.

Luteni Kanali Mketto aliongeza kuwa katika kipindi cha miezi walichokataa wajifunza mambo mengi na kuweza kufuatua tofauli za kuchoma na kujenga Uwanja ambao utatumika michezo ya mpira wa kikapu na tenesi.

Akisoma risala ya wahitimu hao Prisca Mshange alisema kuwa muda unaotolewa kwa mafunzo ni mfupi ni vema ungaongezwa ili waweze kuelimishwa masomo mengi kuliko ilivyo sasa.

Alisema kuwa baada ya mafunzo hayo watakwenda kuwa mabalozi wazuri na kuhamasisha shughuli mbalimbali za kujitegemea na kuwa wazalendo wa kulinda nchi

Kozi ya wanafunzi ilianza juni 12 mwaka huo ambapo wahitimu wameweza kushiriki mafunzo mbalimbali ikiwemo kujitolea kutoa damu , ujenzi wa uwanja wa mpira kwa ajili ya mchezo wa pete, mpira wa mikono na kikapu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi