Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wahifadhi Watakiwa Kulinda Maliasili za Taifa
Aug 30, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Juma Mkomi amewataka Wahifadhi kwenda kusimamia jukumu ya msingi la Wizara ya Maliasili na Utalii ambalo ni kulinda na kuhifadhi maliasili za Taifa ikiwemo misitu na wanyamapori.

 Mkomi ameyasema hayo leo Jumanne Agosti 30, 2022 jijini Arusha wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Wenyeviti wa Sekretarieti na Maafisa wa Kanda kumi za kiikolojia katika nyanja za intelijensia, uchunguzi na mashtaka.

Mafunzo hayo yanayofanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia leo, yamehudhuriwa na washiriki kutoka Jeshi la Polisi nchini, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Wahifadhi kutoka TANAPA, NCAA, TAWA na TFS, 

Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo, Mkomi amesema Wahifadhi wana wajibu wa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama katika kuwabaini majangili wa wanyamapori na misitu

Amewataka washiriki hao kuzingatia mafunzo hayo  na kwenda kuyafanyia kazi kwa kuhakikisha wahalifu wa wanyamapori na misitu wanakamatwa kabla ya kuharibu Maliasili zetu.  

“Mafunzo hayo mtakayopewa yakawe chachu katika kuchagiza utalii, hivi sasa filamu ya Royal Tour imeitangaza vizuri nchi yetu na  Watalii wameanza kumiminika nchini kutokana na kazi kubwa mnayofanya ninyi Wahifadhi, msingekuwa mmefanya kazi kubwa kulinda wanyamapori watalii wasingekuja kwa sababu kusingekuwa na wanyamapori,” amesema.

Kutokana na jukumu walilonalo la kulinda Maliasili, Naibu Katibu Mkuu Mkomi amewataka wahifadhi hao kuzingatia mafunzo hayo hususani suala la uchunguzi kwa kujifunza mbinu za kuzuia uharibifu wowote unaoweza kutokea kwenye maeneo ya hifadhi. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wanyamapori, Dkt. Maurus Msuha amesema suala la Uhifadhi linakabiliwa na changamoto ya usimamizi wa Maliasili hivyo mafunzo hayo yakalete majawabu katika kulinda maliasili

Pia Dkt. Msuha amesema mafunzo hayo yanakwenda kuboresha utendaji kazi kwa kuhakikisha uhalifu wa wanyamapori na misitu litachochea ufanisi zaidi katika utendaji wa kazi wa kulinda maliasili zetu.

Naye Mratibu wa Mafunzo hayo ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Wanyamapori, Robert Mande amesema mafunzo hayo ni muendelezo wa kukumbushana namna ya kushughulika na wahalifu wa wanyamapori wa misitu mara wanapokamatwa.

“Lazima tuhakikishe kuwa tunalinda rasilimali za wanyamapori ili watalii wanavyokuja waweze kuziona na waweze kuwa na usalama”, Mande amefafanua.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi