Mkurugenzi msaidizi anayeshughulikia shughuli za Serikali, Idara ya Tawala za Mikoa Bw. Johnson Nyingi akisisitiza kwa washiriki wa mafunzo ya matumizi ya mfumo wa Epicor 10.2 kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria Kanuni na taratibu, ameyasema hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Injinia Musa Iyombe wakati wa hafla ya kufunga mafunzo hayo leo Jijini Mbeya.
Na: Frank Mvungi- MAELEZO, Mbeya
Washiriki wa mafunzo ya matumizi ya mfumo wa Epicor 10.2 wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu kwa kuzingatia sheria, kanuni , taratibu na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali katika matumizi ya rasilimali fedha wanapotoa huduma kwa wananchi.
Mafunzo hayo yamewashirikisha wahasibu, waweka hazina na maofisa ugavi wa mikoa ya Mbeya, Songwe na Rukwa ambapo yanaendeshwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kushirikiana na PS3 ambao ni mradi unaofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID).
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Injinia Musa Iyombe wakati wa hafla ya kufunga mafunzo hayo leo Jijini Mbeya, Mkurugenzi msaidizi anayeshughulikia shughuli za Serikali, Idara ya Tawala za Mikoa Bw. Johnson Nyingi amesema kuwa wahasibu, na waweka hazina wanalo jukumu kubwa katika kuwahudumia wananchi hivyo mafunzo hayo ni chahu yakuongeza uadilifu na tija.
Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia shughuli za Serikali, Idara ya Tawala za Mikoa Bw. Johnson Nyingi akieleza umuhimu wa uadilifu wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya matumizi ya mfumo wa Epicor 10.2 kwa waweka hazina na wahasibu wa mikoa ya Mbeya, Songwe na Rukwa leo Jijini Mbeya.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya matumizi ya mfumo wa Epicor 10.2 wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi ambaye ni Mkurugenzi msaidizi anayeshughulikia shughuli za Serikali, Idara ya Tawala za Mikoa Bw. Johnson Nyingi ambaye alimuwakilisha Katibu Mkuu Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Injinia Musa Iyombe wakati wa hafla ya kufunga mafunzo hayo leo Jijini Mbeya.
‘’Ni matumaini yangu kuwa mtaenda kutafsiri kwa vitendo mafunzo haya katika maeneo yenu ya kazi hali itakayosaidia kuongeza tija na kuboresha huduma ambapo jambo la muhimu ni kuzingatia thamani ya fedha zinazotumika ili ziendane na huduma wanazopata wananchi” Alisisitiza Bw. Nyingi
Akifafanua, Bw. Nyingi amesema kuwa washiriki wa mafunzo hayo hasa wahasibu na waweka hazina wanawajibika kuhakikisha kuwa malipo yanayofanyika yanaendana na bajeti zilizotengwa katika halmashauri zao na si vinginevyo.
Pia alizitaka halmashauri zote kushirikiana na mikoa yao katika kutatua changamoto zinazojitokeza wakati wa kutoa huduma kwa wananchi kwa kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora.Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo akizungumza wakati wa hafla ya kufungwa kwa mafunzo hayo leo Jijini
Mbeya.
Aidha, aliwaasa washiriki wa mafunzo hayo kutoka mikoa ya Mbeya, Songwe na Katavi kuhakikisha kuwa ripoti na malipo vinatolewa kwa wakati na kusaidia katika kuboresha huduma zinazotolewa.
Katika kuwahudumia wananchi aliwaasa washiriki kuwa washauri wazuri wa viongozi wao katika halmashauri zao ili hatimaye matokeo chanya yapatikane katika huduma wanazotoa kwa wananchi kwa kuzingatia azma ya Serikali kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kutokana na mafunzo hayo aliwataka washiriki hao kuwashirikisha ujuzi waliopata wale ambao hawakuweza kushiriki katika mafunzo hayo kwa maslahi ya wananchi wanaowahudumia.
PS3 ni mradi unaofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID). Mradi huu wa miaka mitano unatekelezwa katika mikoa 13 ya Tanzania bara.
(Picha na Frank Mvungi- MAELEZO, Mbeya)