Na Mwandishi Maluum – Dar es Salaam
Wagonjwa saba wenye tatizo la hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo wamepatiwa matibabu katika kambi maalum ya matibabu iliyofanywa na Wataalamu Mabingwa wa Mfumo wa Umeme wa Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Hospitali ya Shifa iliyopo nchini Misri.
Akizungumzia kuhusu kambi hiyo iliyomalizika hivi karibuni, Daktari Bingwa wa Mfumo wa Umeme wa Moyo kutoka JKCI, Yona Gandye alisema kambi hiyo ya siku mbili ilikuwa maalum kwa ajili ya kutoa tiba kwa wagonjwa pamoja na kutoa mafunzo kwa madaktari na wataalamu wengine wa Taasisi hiyo.
Dkt. Gandye alisema matibabu ya wagonjwa hao waliyagawa katika makundi matatu ambapo kundi la kwanza ni la wagonjwa ambao moyo ulishindwa kufanya kazi ukiambatana na tatizo la hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo unaokwenda taratibu (Heart failure & slow electrical conduction). Wagonjwa hao walipandikizwa kifaa kinachojulikana kwa jina la Cardiac Resynchronical Therapy – CRTD) kinachotumia umeme mkubwa (High Power Device).
“Kifaa hiki cha CRTD ambacho waliwekewa wagonjwa watatu kinasawazisha mgawanyiko wa umeme wa moyo kufanya kazi kwa pamoja (Synchronization). Uwekaji wa kifaa hiki unatumia zaidi ya saa moja kutegemeana na tatizo alilokuwa nalo mgonjwa”, alisema Dkt. Gandye.
Kundi la pili la wagonjwa waliotibiwa katika kambi hiyo ni wale waliokuwa na tatizo la hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo unaosababisha mapigo ya moyo kwenda haraka kuliko kawaida ambapo matibabu yao yalichukuwa zaidi ya masaa mawili.
Dkt. Gandye alisema, “Wagonjwa hawa ambao walikuwa watatu walipata huduma ya matibabu ambayo kwa kitaalamu yanajulikana kwa jina la EP Study & ablation ambapo wataalamu kwa kutumia vifaa maalum vilivyopo katika mtambo wa Carto 3 System 3D & Conventional System wanauwezo wa kutambua sehemu ambayo hitilafu ya umeme inapotokea na kisha kuithibiti ili hali hiyo isitokee tena”.
“Kundi la tatu lilikuwa ni la mgonjwa mmoja kutoka Zanzibar aliyekuwa na tatizo la umeme wa moyo kwenda taratibu (Atrial Fibrillation with slow Ventricular response) na kuwekewa kifaa cha kuusaidia moyo kufanya kazi ambacho kwa jina la kitaalamu kinajulikana kwa jina la Pacemaker”.
Dkt. Gandye alisema hali za wagonjwa zinaendelea vizuri na kuna wagonjwa ambao wamesharuhusiwa na kurudi nyumbani na wengine wataruhusiwa siku chache zijazo.
Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo Prof. Mervat Aboulmaaty kutoka Hospitali ya Shifa iliyopo nchini Misri aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kufunga vifaa tiba vya kisasa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kusomesha wataalamu ambao wanatoa huduma za matibabu ya kibigwa kwa wananchi.
Prof. Mervat alisema kambi hiyo pamoja na kutoa matibabu kwa wagonjwa pia ilienda sambamba na ubadilishanaji wa ujuzi wa kazi pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya ndani na nje ya nchi.
“Wakati tunafanya matibabu ya upandikizaji wa kifaa cha CRTD yalirushwa moja kwa moja kwa njia ya satellite kupitia mtandao wa Zoom kutokea katika mtambo wa Cathlab (Catheterization Laboratory) ambayo ni maabara ya uchunguzi na tiba ya magonjwa ya moyo inayotumia mionzi maalum uliopo hapa JKCI Tanzania ambapo wataalamu 42 waliweza kuona moja kwa moja tulichokuwa tunakifanya”.
“Pia tulitoa mafunzo kwa njia ya mtandao wa Zoom kuhusu matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo na upandikizaji wa kifaa cha CRTD ambapo wataalamu zaidi ya 291 walihudhuria na kuweza kuuliza maswali mbalimbali kwa njia ya ujumbe fupi wa maandishi. Kutoa mafunzo kwa njia hii kunasaidia kwa kiasi kikubwa elimu hii kuwafikia watu wengi zaidi ndani na nje ya nchi”, alisema Prof. Mervat.
Kwa upande wake Sabina Machange ambaye ni mwalimu mstaafu alishukuru kwa huduma alizozipata na kusema kwa muda wa miaka mitatu amekuwa na tatizo la kutokupumua vizuri, kuvimba tumbo na miguu baada ya kufanyiwa uchunguzi wataalamu walimwambia moyo wake haufanyi kazi vizuri na hivyo kutakiwa kuwekewa kifaa cha kuusaidia moyo kufanya kazi vizuri CRTD.
“Jumatano ya tarehe 23 mwezi huu nilifanyiwa upasuaji mdogo na kuwekewa kifaa hiki, sasa hivi ninajisikia vizuri nilikuwa siwezi kuinama kabisa lakini sasa hivi ninainama bila shida, nilikuwa siwezi kupumua vizuri sasa hivi ninapumua bila wasiwasi. Leo hii nimeruhusiwa, Daktari ameniambia nirudi kliniki jumanne ijayo”.
Mama Sabina alisema changamoto kubwa aliyokutana nayo ni gharama kubwa ya matibabu na kuambiwa kuwa bima ya taifa ya afya (NHIF) ambayo anaitumia hailipii matibabu hayo na kuiomba Serikali iangalie ni namna gani itawasaidia wagonjwa wenye matatizo kama yake ili waweze kupata matibabu.
“Niliambiwa gharama ya kuwekewa kifaa hiki ni shilingi milioni 29 na laki mbili nikaenda Makao Makuu ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Dodoma na kuwaandikia barua ili wanilipie nusu gharama wakanijibu kwa barua kuwa utaratibu huo haupo”,.
“Lakini ndugu na jamaa zangu walinichangia fedha, nikaweza kulipia nikawekewa kifaa hiki. Ninaiomba Serikali kupitia mfuko huo ishiriki kulipia hata kwenye matibabu yenye gharama kubwa kwa kuchangia japo nusu gharama”, alisema Mama Sabina.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Prof. Mohamed Janabi alimshukuru Prof. Mervat na timu yake ya madaktari wawili kutoka nchini Misri kwa huduma waliyotoa kwa wagonjwa na kuweza kuokoa maisha yao.
“Ninawashukuru Madaktari, Wauguzi pamoja na Mafundi Sanifu wa Moyo (Technician) wa Cathlab kwa ushirikiano mzuri waliouonesha kwa wageni wetu pamoja na kupokea mafunzo yaliyotolewa na wataalamu hao pia kwa huduma nzuri waliyoitoa kwa wagonjwa ambao walipatiwa matibabu katika kambi hii”, alishukuru Prof. Janabi.