Jumla ya wagonjwa 20 ambao ni watu wazima wamefanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua katika kambi maalum ya matibabu ya moyo ya siku sita iliyofanywa na madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Hospitali ya Saifee ya mjini Mumbai nchini India
Wagonjwa hao wamefanyiwa upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo (CABG – Coronary Artery Bypass Grafting) tumefanya kwa wagonjwa nane (8), kubadili valvu mbili za moyo (Valve Replacement) kwa wagonjwa 10, upasuaji wa kurekebisha mshipa mkubwa unaotoa damu kwenye moyo kwenda sehemu zote za mwili (Aortic Aneurysm Repair/Bental Procedure) na mgonjwa mmoja alitolewa damu iliyokuwa imeganda kwenye mshipa wa moyo (Blood Clot).
Wagonjwa wote waliofanyiwa upasuaji hali zao zinaendelea vizuri na wote wameruhusiwa kutoka katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) na kupelekwa wodini kwa ajili ya kuendelea na matibabu pamoja na kufanya mazoezi. Ndani ya siku chache zijazo tutaanza kuwaruhusu baadhi ya wagonjwa ambao hali zao zimeimarika kurudi nyumbani.
Aidha katika kambi hiyo iliyoanza tarehe 18 hadi tarehe 23 mwezi huu wa Juni kwa mara ya kwanza tumefanya upasuaji wa kuvuna mshipa wa damu ndani ya kifua upande wa kulia na kushoto na kuunganisha kwenye misuli ya moyo ili kuuongezea moyo damu.
Kambi hiyo pia ilienda sambamba na utoaji wa elimu pamoja na kubadilishana ujuzi wa kazi kati ya wageni na madaktari wetu pamoja na wauguzi.
Changamoto kubwa tunayokabiliana nayo ni wagonjwa wengi tunaowapokea mioyo yao kutokuwa katika hali nzuri hivyo basi tunawaomba wananchi kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara hii itawasaidia kujuwa kama wana matatizo ya moyo au la na kama wanamatatizo wataweza kupata tiba kwa wakati.
Kutokana na matibabu ya moyo kuwa ya gharama kubwa tunaendelea kuwasisitiza wananchi wajiunge na mifuko ya bima ya afya ambayo itawasaidia kulipa gharama za matibabu pindi watakapohitaji kutibiwa. Pia itasaidia Hospitali yetu kuendelea kujiendesha yenyewe kwa kushirikiana na Serikali na wadau wengine.
Tunawaomba wananchi waendeleee kuchangia damu kwani wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa moyo wanahitaji kuongezewa damu kati ya chupa sita (6) hadi saba (7) wakati wanapatiwa matibabu. Taasisi inamkaribisha mtu mmoja mmoja au kikundi cha watu ambao wanapenda kuchangia damu waweze kufanya hivyo ili tuokoe maisha ya ndugu zetu wanaohitaji kufanyiwa upasuaji wa moyo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Uhusiano
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
27/06/2018