Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wagonjwa 10 Wazibuliwa Mishipa ya Damu Iliyoziba
Aug 11, 2023
Wagonjwa 10 Wazibuliwa Mishipa ya Damu Iliyoziba
Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na Mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakishirikiana na mwenzao kutoka Hospitali ya Max iliyopo nchini India, Dkt. Subhash Sinha kupandikiza mshipa wa damu katika moyo wakati wa kambi maalum ya siku saba ya matibabu ya moyo kwa wagonjwa ambao mishipa yao ya damu imeziba na kiwango cha ufanyaji kazi wa moyo kipo chini ya asilimia 30. Jumla ya wagonjwa 10 wamepatiwa matibabu katika kambi hiyo iliyoanza jumatatu na kumalizika leo jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Maalumu – Dar es-salaam

10/08/2023 Wagonjwa 10 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa kuzibua mishipa ya damu iliyoziba katika kambi maalumu ya matibabu ya moyo ya siku saba.

 

Kambi hiyo iliyomalizika leo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam, imefanywa na madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa JKCI kwa kushirikiana na mwenzao kutoka Hospitali ya Max iliyopo nchini India.

 

Akizungumzia kambi hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Upasuaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Angela Muhozya alisema kambi hiyo imefanyika kwa mara ya nne kwa kushirikiana na wataalam kutoka Hospitali ya Max kuwafanyia upasuaji wagonjwa waliohitaji utaalam zaidi kutokana na mioyo yao kuwa na uwezo mdogo wa kufanya kazi.

 

Dkt. Angela alisema kambi hiyo ililenga kufanya upasuaji mkubwa wa moyo kwa watu wazima ambao wana mishipa ya moyo iliyoziba lakini pia viwango vya ufanyaji kazi wa mioyo yao kuwa chini ya asilimia 30.

 

“Upasuaji ambao tumewafanyia wagonjwa hawa ni mgumu kidogo, tumekuwa tukiwafanyia uchunguzi wagonjwa hawa na kuwakaribisha wenzetu kutoka Hospitali ya Max ili kwa pamoja tuweze kuwahudumia wagonjwa hawa lakini pia tuweze kuongeza ujuzi wetu katika kuwahudumia wagonjwa wa aina hii”, 

 

“Katika kambi hii wagonjwa wamepandikizwa mishipa ya moyo mitatu na wengine zaidi ya mitatu bila ya kuusimamisha moyo kwa mafanikio makubwa hii kwetu sisi ni hatua kubwa katika kutoa huduma kwa wagonjwa wa moyo”, alisema Dkt. Angela

 

Aidha, Dkt. Angela alisema JKCI inategemea kufanya upasuaji wa mshipa mkubwa wa moyo ambao umetanuka, kubadilisha mishipa ya moyo pamoja na kuweka mlango mpya kwa wagonjwa ambao wana matatizo ya mishipa mikubwa ya moyo kutanuka.

Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kutoka Hospitali ya Max iliyopo nchini India, Subhash Sinha alisema ushirikiano wake na wataalam wa JKCI unaonyesha mafanikio makubwa tangu walipoanza kushirikiana hadi sasa.

 

Dkt. Sinha alisema kupitia upasuaji wa moyo ambao amekuwa akifanya na wataalam wa JKCI amekuwa pia akitoa mafunzo na mbinu mbalimbali za kufanya upasuaji mkubwa wa mishipa ya moyo kwa wagonjwa ambao mapigo yao ya moyo yapo chini ya asilimia 30 bila ya kuusimamisha moyo.

 

“Ujio wangu hapa JKCI kwa kawaidia huwa ni wa wiki moja, naamini hizi wiki moja moja ninazokuja kuwasaidia wagonjwa kupata matibabu wataalam wa JKCI nao hupata nafasi ya kujifunza kwani sasa naona mabadiliko makubwa wakati tunafanya upasuaji”, alisema Dkt. Sinha.

 

Dkt. Sinha alisema anatamani siku moja JKCI iwe Taasisi kubwa Afrika inayotegemewa na wagonjwa wa moyo waliopo Afrika kwani gharama za matibabu ni za kawaida tofauti na zile zinazotolewa nje ya Afrika lakini pia uwekezaji wa vifaa tiba vilivyopo katika Taasisi hiyo vinajitosheleza kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo. 

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi