Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wafugaji Wanaolisha Mifugo katika Mashamba ya Wakulima Kukamatwa
Jul 03, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mbaraka Kambona, Lindi

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack kuhakikisha anawakamata Wafugaji wote wanaopiga Wakulima na kulisha mifugo yao katika mashamba yenye mazao.

Ndaki alitoa maelekezo hayo wakati wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua migogoro ya Wafugaji na Wakulima aliyoifanya katika Wilaya za Kilwa na Liwale, mkoani Lindi Julai 2, 2022.

Alisema kuwa wafugaji wengi hasa wanaohamahama kutafuta malisho ndio wanaolalamikiwa na wakulima kuwa wao ndio chanzo cha vurugu, wanawapiga wakulima na kulisha mifugo yao kwa ubabe katika mashamba ya wakulima hao.

Aliongeza kwa kusema kuwa vitendo vya ubabe vinavyofanywa na baadhi ya wafugaji havikubaliki huku akisisitiza kuwa nchi haiwezi kuwa na jamii ya namna hiyo na hivyo wale wote wanaofanya vitendo hivyo hawatavumiliwa.

"Sasa Mkuu wa Mkoa na timu yako naomba wale wote wanaopiga na kulisha mifugo katika mashamba ya wakulima wakamatwe kuanzia leo hii wawekwe ndani na wafunguliwe mashtaka ili sheria ichukue mkondo wake," alisema Ndaki

Kufuatia maelekezo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack alichukua hatua za haraka na kuwaelekeza wakuu wa vituo vya Polisi katika Wilaya ya Kilwa na Liwale kuwakamata wafugaji waliowapiga wakulima na apatiwe taarifa ya utekelezaji wake haraka.

"Yupo kijana alimpiga Diwani hapa Kata ya Kimambi na amemlipa laki tatu na nusu (350, 000), nasema hiyo ni dharau na haikubaliki, nakuagiza OCD upo hapa nataka uondoke na huyo aliyemlipa Diwani na wale wote wanaohusika na vitendo hivyo wakamatwe leo ," alisisitiza

Aliongeza kwa kusema kuwa wafugaji wote walioingia bila utaratibu mkoani humo waanze kuondoka wenyewe kabla hawajaanza kushughulikiwa kwa sababu wao ndio chanzo cha vurugu.

"Afisa Mifugo na Mtendaji wa Kata nataka kuona wafugaji wote walioingia kinyemela wanaanza kuondoka na wafugaji wengine mnaobaki mkiendekeza vitendo hivi nataka niwahakikishie nitawaondoa mmoja baada ya mwingine," alifafanua

Mmoja wa Wafugaji wilayani Kilwa, Kidole Hababa alisema ili vitendo hivyo viweze kukomeshwa ni muhimu Serikali ikawaita Wazee wa Wafugaji ili washirikiane nao kwa sababu wazee hao wanawafahamu vijana wanaofanya vitendo hivyo watatumia njia zao za kimila kuwawajibisha.

Aidha, katika hatua nyingine, Waziri Ndaki aliwataka Wafugaji kushiriki kikamilifu katika zoezi la kusajili mifugo yao huku akiwahimiza kuanza kumiliki maeneo yao ya kufugia akiamini kuwa wakifanya hivyo itasaidia kupunguza migogoro kwa kiasi kikubwa.

Halikadhalika alitumia fursa hiyo pia kuwataka Watendaji wa Kata na Wenyekiti wa vijiji kujitafakari kwa sababu baadhi yao wanalalamikiwa kuwa sio waadilifu na kuwa ni sehemu ya migogoro hiyo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi