Prisca Ulomi na Faraja Mpina, WHMHT, Dodoma
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amewataka wafanyakazi wa Wizara anayoiongoza kutambua kuwa wao ni sehemu ya kuipeleka Tanzania Kidijitali kwa kuwa wana wajibu, majukumu na dhamana ya kutekeleza sera, sheria, kanuni, miongozo na miradi ya kitaifa ya Sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
Waziri Nape ameyasema hayo leo wakati akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika jijini Dodoma ambapo amewaarifu wajumbe wa mkutano huo kujitambua kuwa wao ni kiungo muhimu kati ya Menejimenti ya Wizara na wafanyakazi hivyo ni vema kiungo hicho kusimamiwa vizuri kwa kuwa Wizara hiyo inaangaliwa na kufuatiliwa kwa karibu kuliko Wizara nyingine kuendana na dhamana ambayo imepewa ya kuipeleka Tanzania kidijitali
Ameongeza kuwa wafanyakazi hao ni sehemu ya Tanzania tunayoitaka na kutoa wito kwa Menejimenti ya Wizara kuhakikisha inaweka mazingira mazuri mahala pa kazi ili wafanyakazi waweze kutekeleza vema majukumu yao.
“Mimi ni muumini wa haki kwa kuwa maisha niliyopitia yamenifundisha, tujifunze kutenda haki, ukiona kwenye moyo wako huwezi kutenda haki, Wizara hii sio mahali pako, hivyo niwatake viongozi na wafanyakazi tupendane kwa kuwa upendo unatibu na natambua kila mmoja ana changamoto zake na sio rahisi kutimiza kila hitaji lakini jibu ni upendo,” amesisitiza Waziri Nape.
Naye Mwenyekiti wa baraza hilo ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi amezungumzia utekelezaji wa anwani za makazi kuwa ni jukumu kubwa la Wizara kwa sasa na kuwataka wafanyakazi kuona fahari kuwa sehemu ya utekelezaji kwa weledi na kuacha historia kwa kuwa utekelezaji wa mfumo huo utaifungua nchi kuingia kwenye uchumi wa kidijitali
Naibu Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Rugemalira Rutatina amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kujali maslahi ya wafanyakazi nchini pamoja na uongozi wa Wizara kwa kutimiza takwa la kisheria na kufanya baraza la wafanyakazi.
Naye Mwenyekiti wa Tawi la TUGHE wa Wizara hiyo akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wa Wizara hiyo, Laurencia Masigo amesema kuwa anashukuru uongozi wa Wizara hiyo kwa kujali wafanyakazi na kwa sasa hawana malalamiko wala hoja iliyowasilishwa kwenye uongozi wa Baraza hilo ambapo hii inadhihirisha kuwa mahali pa kazi kuna amani, umoja na ushirikiano na kufanya kazi katika timu moja ndio nguzo ya mafanikio.
Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya wajumbe wa Baraza hilo, Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dodoma, Samwel Nyungwa amemuahidi Waziri Nape kuchapa kazi kama alivyoelekeza na kuhakikisha taswira ya Wizara hiyo inaendelea kung’aa.
Mkutano wa Baraza unafanyika kwa siku mbili jijini Dodoma ambapo wajumbe watapitia taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya mwaka wa fedha 2021/2022; na mpango wa bajeti wa Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023.