Na Mwandishi Wetu.
Chama cha wasafirishaji wanyamapori hai nje ya nchi kibiashara (TWEA) kimeiomba serikali isitishe zuio la kusafirisha nje wanyamapori hao ili wanachama wake waweze kujikwamua na hali ngumu ya maisha inayaowakabili.
Wakizungumza mbele ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga kwenye kikao cha Wizara na wawakilishi wa wafanyabiashara hao waliiomba serikali isikilize kilio chao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama hicho, Enock Balilemwa alisema baadhi ya wanachama wakiwemo walemavu waliokuwa wamechukua mikopo benki wamefukuzwa kwenye nyumba zao baada ya kushindwa kufanya marejesho ya mikopo hiyo kufuatia zuio la biashara hiyo.
Alieleza kuwa baadhi ya wanachama wake wamejikuta kwenye hali ngumu ya kupoteza mali zao na kuingia kwenye mifarakano na wateja wao kwa vile wafanyabiashara hao walichukua pesa toka kwa wateja kama malipo ya awali hivyo wakati wa zoezi la kusimamisha biashara linafanyika liliwakuta wafanyabiashara hao wameshachukua pesa za wateja wao kama malipo ya awali.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa TWEA, Fatuma Hamis alimweleza Naibu Waziri kuwa zuio hilo lilifanywa ghafla mno bila kutoa muda kwa wafanyabiashara hao ukizingatia kuwa walikuwa wakimiliki leseni halali walizokuwa wamezilipia pesa bila kuzifanyia kazi ya kuwaingizia kipato.
Aidha, alimweleza Naibu Waziri huyo kuwa zuio hilo limepelekea wafanyabiashara hao kupoteza uaminifu kwa wateja wao na kuwaweka kwenye mazingira magumu ya ushindani kibishara kwani biashara hiyo haifanywi na Tanzania pekee.
Wakati akijibu hoja za Wafanyabiashara hao, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga amekihakikishia Chama cha Wasafirishaji Wanyamapori Hai nje ya nchi kibiashara (TWEA) kuyafanyia kazi malalamiko yao kadri itakavyowezekana na kuja na kauli moja ya Serikali.
Amesema lengo la Serikali la kuzuia usafirishaji wanyamapori hao lilikuja baada ya wafanyabishara ambao sio waaminifu kukengeuka kwa kuanza kujihusisha na ujangili pamoja na kusafirisha wanyamapori ambao hawamo kwenye orodha ya vibali walivyopewa.
“Dhumuni la serikali la kusitisha biashara hii ilikuwa ni njema tu baada ya kuona wajanja wachache wananufaika huku wanyonge wakibaki watazamaji kwenye rasilimali zao’’ alisema Hasunga.
Hata hivyo, Naibu Waziri Hasunga alisema lengo la Serikali halikulenga kuwakomoa bali ni kutaka kuweka mfumo mzuri utakaomsaidia kila Mtanzania aone ananufaika na rasilimali za nchi yake.
“Nimewasikiliza kwa umakini wa hali ya juu lakini hata hivyo Serikali ina utaratibu wake wa kutoa majibu, tupeni muda ili tukitoa majibu kuhusu hoja zenu kuwe na jibu moja kwa kila mmoja wetu’’ aliongeza Hasunga.
Katika hatua nyingine, Hasunga aliwataka wafanyabishara hao wasisite kuonana nae muda wowote ule kwa kumpigia simu au kwa kuonana nae pindi wanapokuwa na jambo la kutaka kuzungumza nae kwa ajili ya manufaa mapana ya Wizara na nchi kwa ujumla.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya wanyamapori, Dkt. Nebbo Mwina aliwahakikishia wafanyabiashara kufanyia kazi malalamiko yao kutokana na hoja za msingi zilizowasilishwa na wafanyabiashara hao.
“Nimesikia baadhi ya malalamiko yenu ambayo kwa nafasi yangu niliyo nayo kwa kushirikiana na watumishi walio chini yangu, nitayashughulikia” alisema Dkt. Nebbo.