Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Mobhare Matinyi amebainisha kuwa, Serikali ipo katika mchakato wa mapitio ya Sera ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003 ambapo imekusudia kushirikisha wadau mbalimbali ikiwemo Mashirika ya Serikali, Vyombo vya Habari, Asasi za Kiraia, Wasomi, Washirika wa Maendeleo na wadau wengine muhimu.
Bw. Matinyi ameyasema hayo leo mjini Morogoro, wakati akizindua kikao kazi cha mapitio ya sera hiyo kilichoandaliwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Idara ya Habari (MAELEZO) kwa kushirikiana na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO).
Aidha amebainisha kuwa, katika mchakato huo, hatua mbalimbali zitafanyika ikiwemo uchambuzi wa kina wa sera iliyopo, utafiti wa kitaaluma, na kuzingatia viwango bora vya kimataifa katika vyombo vya habari na utangazaji.
“Vilevile mafunzo na mashauriano ya wadau yatafanyika kwa maafisa wanaohusika na mapitio ya sera pamoja na mashauriano na wadau husika ili kukusanya michango na mapendekezo yao, uchambuzi wa sera za nchi nyingine ili kupata uzoefu na kutambua mbinu bora za kimataifa, kufanya tathmini ya utekelezaji wa sera ili kupima ufanisi wa sera katika kukuza uhuru wa vyombo vya habari na kutathmini mfumo wa kisheria na udhibiti ili kuhakikisha inaendana na malengo ya sera,” ameeleza Bw. Matinyi.
Katika hatua hiyo, Bw. Matinyi amesema Mapitio ya Sera ya Habari na Utangazaji iliyodumu kwa miaka ishirini ni hatua muhimu katika kuhakikisha tasnia ya habari inabaki kuwa hai, shirikishi na inayowiana na mahitaji ya kisasa.
Aidha, mapitio hayo yatarahisisha utangazaji wa uhuru wa vyombo vya habari, upatikanaji wa habari, usalama wa wanahabari na ushirikishwaji wa kidijitali huku ikizingatia dhamira ya Tanzania katika kukuza maadili ya kidemokrasia na haki za binadamu.
“Maendeleo ya teknolojia ya sasa yanaathiri kwa kiasi kikubwa jinsi vyombo vya habari, sekta ya habari na utangazaji na mashirika yanavyofanya kazi. Sera inahitaji kuhuishwa ili iendane na mabadiliko ya teknolojia mpya, usalama wa kidijitali na maswala ya faragha. Aidha, mapitio ya sera yatafichua maeneo ambayo sera haijawa na ufanisi katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu yaliyokusudiwa na marekebisho yatafanywa ili kuboresha utendaji na matokeo chanya,” amefafanua Bw. Matinyi.
Kikao kazi hicho kimewashirikisha wadau mbalimbali wa Sekta ya Habari na Haki za Binadamu ndani na nje ya serikali.