Na Shamimu Nyaki
Ofisi ya Hakimiliki nchini (COSOTA ) imetekeleza Agizo la Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa la kutaka kutoa Semina kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria ndogo kuhusu utekelezaji wa mabadiliko ya Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ya Mwaka 2022.
Semina hiyo imefanyika Septemba 20, 2022 Bungeni Dodoma ambapo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Saidi Yakubu amemuwakilisha Mhe. Waziri Mchengerwa katika Semina hiyo, ambayo pia imehusu Rasimu ya ukusanyaji wa Ada kwa vibebeo (Blank Tape Levy).
Akizungumza katika Semina hiyo, Naibu Katibu Mkuu Yakubu amesema Serikali imefanya marekebisho hayo ili kunufaisha wadau wa kazi za Sanaa kutokana na kazi kubwa wanayofanya ya kutoa burudani na kuchangia Pato la Taifa.
"Vifaa vilivyopendekezwa kubebea kazi za Sanaa ikiwemo simu janja, flash, Laptop na vingine vimeonekana kusaidia kuongeza mapato kwa Wasanii kutokana na kuwa na watumiaji wengi, ambapo Utafiti umefanywa katika baadhi ya nchi ikiwemo Afrika Kusini, Nigeria na Algeria, hivyo Sheria hii inaleta ahueni kwa Wasanii wetu", amesema Ndugu Saidi Yakubu.
Ameongeza kuwa, Semina hiyo imetolewa kwa Waheshimiwa Wabunge kwa kuwa wao ni wawakilishi wa wananchi na wana nafasi kubwa ya kuelimisha Wasanii katika maeneo yao.
Akiwasilisha Marekebisho ya Sheria hiyo, Mwanasheria wa Hakimiliki nchini, Bw. Zephania Lyamuya Doreen Sinare ameeleza kuwa pamoja na mambo mengine, mabadiliko hayo yatasaidia kusimamia uendeshwaji wa kampuni za ukusanyaji na ugawaji wa Mirabaha, kutunza rejista ya kazi za ubunifu na kupambana na uharamia.
Wakichangia katika Semina hiyo, Waheshimiwa Wabunge wamepongeza marekebisho hayo ambayo yametoa fursa ya kukuza na kuongeza pato la Wasanii ambapo pia wametoa ushauri utekelezaji wa Sheria hiyo kugusa Wasanii wengi