Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Vyama vya Ushirika 5,424 Vyasajiliwa MUVU
Aug 11, 2023
Vyama vya Ushirika 5,424  Vyasajiliwa MUVU
Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson Ndiege akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu mafanikio ya Sekta ya Ushirika na Mpango wa Kuimarisha Ushirika kwa Mwaka 2023/24 leo Agosti 11, 2023 kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dodoma.
Na Lilian Lundo - MAELEZO

Vyama vya Ushirika 5,424 kati 7,300 vimesajiliwa katika Mfumo wa Kidijitali wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU), unaolenga kurahisisha usimamizi na uendeshaji wa Vyama vya ushirika kwa nia ya kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji.

Hayo yameelezwa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson Ndiege katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO jijini Dodoma wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya tume hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/23 na vipaumbele vyake kwa mwaka wa fedha 2023/24.

“Tume kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) imetengeneza Mfumo wa Kidijitali wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU), unaolenga kurahisisha usimamizi na uendeshaji wa Vyama vya Ushirika kwa nia ya kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji, sambamba na kuboresha utendaji,” amesema Dkt. Ndiege.

Ameendelea kusema kuwa, mfumo huo unasaidia kupunguza gharama za uendeshaji, kuwa na uhakika wa kupata takwimu na kuimarisha utendaji/uendeshaji wa Vyama, ambapo hadi kufikia Juni 2023, vyama vya Ushirika 5,424 kati 7,300 vimesajiliwa katika mfumo huo.

Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa  Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson Ndiege akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya Sekta ya Ushirika na Mpango wa Kuimarisha Ushirika kwa Mwaka 2023/24 leo Agosti 11, 2023 kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dodoma.

 

Aidha, tume hiyo kwa kushirikiana na Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala, Bodi za Mazao Nchini Soko la Bidhaa Tanzania, Sekretarieti za Mikoa, Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Halmashauri za Wilaya, Miji na Majiji, Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na wadau wengine, katika mwaka 2022/2023 imeratibu na kusimamia uendeshwaji wa minada, masoko na mauzo ya mazao ya wakulima kupitia Vyama vya Ushirika Nchini.

“Hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2023, jumla ya kilo 1,826,850,970 (sawa na tani 1,826,850.97) zenye thamani ya shilingi trilioni 1.75 ziliuzwa kutoka kwenye mazao ya tumbaku, korosho, pamba, kahawa, ufuta, kakao, mkonge, chai, mbaazi, soya, zabibu, miwa na maharage,” amesema Dkt. Ndiege.

Kwa mwaka huu wa fedha 2023/24 Tume ya Maendeleo ya Ushirika imejipanga kutekeleza maeneo saba ya kimkakati ambayo ni uwekezaji katika mifumo ya kisasa ya kidijitali ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji katika Vyama vya Ushirika, pamoja na Mamlaka za Usimamizi, kuharakisha mchakato wa uanzishwaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika ili kuviwezesha Vyama vya Ushirika kupata Mikopo yenye Riba nafuu.

Vile vile, kuhamasisha mfumo wa ushirika kujiendesha kibiashara wenye kuaminika na shindani ukijikita kwenye kuongeza thamani ya uzalishaji katika Vyama pamoja na kuboresha Sera, Sheria na usimamizi wa ushirika ili kuchochea ukuaji na maendeleo ya Ushirika imara Tanzania.

Pia imejipanga kuhamasisha ushirika kwenye sekta mbalimbali na makundi maalum ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wananufaika na mfumo wa ushirika, kuimarisha uwekezaji wa mali za Ushirika katika uzalishaji pamoja na kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutatua changamoto zilizopo kwenye Ushirika.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi