Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito kwa Vyama na Mashirikisho ya Michezo kutoa nafasi kwa Wanawake kugombea nafasi za uongozi na viwaamini kuwa wanaweza kuongoza nafasi hizo.
Mhe. Gwajima ametoa wito huo leo Oktoba 21, 2023 Jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha Tamasha la Michezo kwa Wanawake (Tanzanite Women Sports Festival), ambapo amesema Tamasha hilo limekua jukwaa kuwakutanisha Wanawake kufurahia mafanikio yao katika michezo.
"Michezo ni Afya na Uhai, ni jukumu la kila mmoja kushiriki katika michezo. Wanawake katika siku za hivi karibuni tumekua tukililetea heshima Taifa letu kupitia michezo ya ndani na ya Kimataifa ikiwemo Mashindano ya CECAFA na Kombe la Dunia," amesisitiza Mhe. Gwajima.
Awali akimkaribisha Mhe.Waziri Gwajima, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Gerson Msigwa amesema. Wizara hiyo itashirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kuitangaza Tanzania kupitia michezo, kuanzisha vituo vya Utamaduni na Michezo nchi nzima.
Katibu Mkuu Msigwa amesisitiza kuwa wale waliovamia maeneo ya michezo wanatakiwa waondoke wenyewe kwa kuwa Serikali imepanga kuyaendeleza maeneo hayo ili yatumike katika michezo.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo Tanzania, Bi. Neema Msitha amesema lengo la Tamasha hilo ni kuhamasisha Wanawake washiriki katika michezo pia kusherehekea mafanikio ambayo wameyapata katika michezo.
Bi. Neema amesema Tamasha hilo limekua na mada mbalimbali za kutoa elimu ikiwemo Uongozi na Utawala wa Wanawake katika michezo, mtazamo wa jamii juu ya ushiriki wa Wanawake katika michezo pamoja na uzoefu wa mchango wa michezo katika ukuaji na uendelezaji wa Wanawake kiuchumi.