[caption id="attachment_53257" align="aligncenter" width="750"] Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi akikagua Uwanja wa Jamhuri Dodoma Juni 15, 2020 ikiwa ni muendelezo wa ziara alizozifanya katika mikoa mbalimbali ili kujiridhisha maeneo mbalimbali wanavyoupokea wanavyoutafsiri, kuuelewa na kutekeleza mwongozo wa Afya Michezoni[/caption]
Na Eleuteri Mangi, WHUSM- Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi amesisitiza kuzingatiwa kwa Muongozo wa Afya Michezoni ili kulinda usalama wa afya za wachezaji, viongozi na mashabiki wakati mechi mbalimbali zinazoendelea kuchezwa nchini.
Dkt. Abbasi ameyasema Juni 15, 2020 jijini Dodoma wakati akikagua uwanja wa Jamhuri ikiwa ni muendelezo wa ziara alizozifanya katika mikoa mbalimbali kama kiongozi wa wizara kujiridhisha na maeneo mbalimbali wanavyoupokea wanavyoutafsiri, kuuelewa na kutekeleza mwongozo wa Afya Michezoni.
Katika ziara hizo, Katibu Mkuu amekuwa akikutana na na wadau mbalimbali wa michezo ikiwemo soka katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Singida, Tanga, Dar es salaam na Dodoma Makao Makuu ambapo Juni 17, 2020 utachezwa mchezo dhidi ya timu ya Yanga na JKT Tanzania kwa lengo la kukumbushana kuhusu Mwongozo na kupeana ufafanuzi kwenye changamoto zinazojitokeza michezoni.
[caption id="attachment_53259" align="aligncenter" width="781"] Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi (kushoto) akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kukagua Uwanja wa Jamhuri Dodoma Juni 15, 2020 ikiwa ni muendelezo wa ziara alizozifanya katika mikoa mbalimbali ili kujiridhisha maeneo mbalimbali wanavyoupokea, wanavyoutafsiri, kuuelewa na kutekeleza mwongozo wa Afya Michezoni.[/caption]Katika kuhakikisha usalama afya unaendelea kusimamiwa, Katibu Mkuu ameutaka uongozi wa michezo mkoa wa Dodoma pamoja na uwanja wa Jamhuri kuhakikisha wachezaji, viongozi pamoja na masabiki wanatumia vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa Covid-19 wakati wa mazoezi pamoja na mechi zitakazochezwa ikiwemo kunawa kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vipukusi, kupimwa joto na mashabiki kukaa kwa kuachiana umbali wa mita moja na kusisitiza atakayekiuka taratibu hizo hatua kali zitachukuliwa ikiwemo kufungwa kwa kiwanja husika kwa mujibu wa Sheria ya Afya ya Umma.
“Fanyeni tathimini na mjiridhishe kwa ukubwa wa uwanja na idadi ya mashabiki wanaotakiwa kuingia, ni vema idadi ya mashabiki iwe nusu wa idadi halisi wanaotakiwa kuingia kiwanja husika inapochezwa mechi kwa kufuata utaratibu maalam wa kujihadhari na Covid-19 na Serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya watakaokiuka Muongozo wa Afya Michezoni”
“Serikali imeahidi na kusisitiza uwanja au eneo lolote la michezo ambapo tutaona ukiukwaji mkubwa wa kanuni za afya michezoni, huo uwanja utafutwa” amesisitiza Dkt. Abbasi.
Amewataka mashabiki na wapenda michezo nchini wawe na tabia ya kukata tiketi mapema hatua itakayowafanya waweze kwenda viwanjani mapema ili kuondoa misongamano kwenye mageti ya viwanja kabla ya mechi kuanza kuchezwa.
[caption id="attachment_53258" align="aligncenter" width="750"] Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi (katikati) akiongea na wadau wa michezo wakati alipofanya ziara ya kukagua Uwanja wa Jamhuri Dodoma Juni 15, 2020 ikiwa ni muendelezo wa ziara alizozifanya katika mikoa mbalimbali ili kujiridhisha maeneo mbalimbali wanavyoupokea wanavyoutafsiri, kuuelewa na kutekeleza mwongozo wa Afya Michezoni. Wa kwanza kushoto ni Afisa Usalama wa Viwanja nchini kutoka Jeshi la Polisi Makao Mkuu Inspekta Hashim Abdala.[/caption]Aidha, Katibu Mkuu amempongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwa na msimamo thabiti wa kusimamia suala la Covid-19 nchini ambapo Mei 28, 2020 aliagiza Wizara zenye dhamana na Afya na Michezo kuandaa mwongozo utakaosaidia kulinda afya za wanamichezo, mashabiki na watanzania.
Mwongozo huo uliosainiwa na Waziri wa afya maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu pamoja na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe unahusisha elimu kwa wadau wa michezo kuhusu kujikinga na maambukizi; kambi, viwanja na mechi; usalama wa wachezaji, na viongozi; mazingira mengine wakati wa mazoezi na mashindano; vifaa vya michezo pamoja na mawanda na kuanza kutumika kwa Mwongozo.
Naye Afisa Michezo Mkoa wa Dodoma Patrick Moshi pamoja na Afisa Usalama wa Viwanja nchini kutoka Jeshi la Polisi Makao Mkuu Inspekta Hashim Abdala wamemhakikishia Katibu Mkuu kuwa hatua zote muhimu kulingana na Mwongozo wa kuzingatiwa wakati wa uendeshaji wa michezo katika kipindi chote cha mlipuko wa Covid-19 utazingatiwa kwa manufaa ya kulinda afya za wachezaji, mashabiki na Watanzania kwa ujumla.