Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Vitambulisho vya Waandishi wa Habari Kutolewa Kidijitali – Msigwa
Mar 16, 2025
Vitambulisho vya Waandishi wa Habari Kutolewa Kidijitali – Msigwa
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo miradi inayotekelezwa na Serikali ya Awamu Sita leo Machi 16, 2025, katika Bandari Kavu ya Kwala, mkoani Pwani.
Na Lilian Lundo - MAELEZO

Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Wizara ya Habari kupiti Idara ya Habari-MAELEZO kwa kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao (e-GA) inaendelea na kukamilisha ujenzi wa mfumo wa usajili na utoaji wa vitambulisho vya kidijitali kwa Waandishi wa Habari.

Msigwa amesema hayo leo Machi 16, 2025 katika Bandari Kavu ya Kwala mkoani Pwani wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari uliojikita kueleza miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita.

“Mfumo wa usajili na utoaji wa vitambulisho vya kidijitali kwa Waandishi wa Habari unalenga kurahisisha, kuongeza uwazi na kuimarisha utendaji kazi wa Waandishi wa Habari kwa kuwapatia huduma ya usajili na utoaji wa vitambulisho vya kazi katika maeneo yao bila kulazimika kusafiri kuja Dodoma au Dar es salaam kupata huduma hii,” amefafanua Msigwa.

Ameendelea kusema kuwa, huduma hiyo itapatikana kwa Waandishi wa Habari watakaokuwa wamekidhi vigezo vya kitaaluma (Taaluma ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma). Aidha, Mwandishi wa Habari atapaswa kujaza taarifa zake na kufuata maelekezo yaliyoko kwenye mfumo ili aweze kujisajili.

“Mfumo huu pamoja na mambo mengine utakuwa na uwezo wa kusajili, kuhakiki na kuhifadhi taarifa za Waandishi wa Habari wote nchini. Mwandishi wa habari atakuwa uwezo wa kujaza taarifa na kuweka mambo muhimu kama vile picha, mahali anapofanya kazi, taarifa za uraia wake n.k,” amefafanua Msigwa.

Aidha, mfumo huo utakuwa na uwezo wa kutoa alama za usalama ambazo mtu hawezi kughushi. Pia, kupitia mfumo huo Mwandishi wa Habari atakua na uwezo wa kuomba na kupata kitambulisho chake “physical ID”. Mfumo utakuwa na uwezo wa kuonesha taarifa kwenye ukurasa wa nyuma “back-end” ambazo zitahakikiwa na kutumiwa na Idara ya Habari kutoa kitambulisho (Press Card) kwa njia ya mtandao.

Vilevile mfumo huo utakuwa na uwezo wa kumpatia Mwandishi wa Habari namba ya malipo “control Number” ya kulipia mtandaoni, na baada ya kulipia, malipo yake yataonekana na kupitishwa na mamlaka husika.
Mfumo huo utakuwa na eneo la waombaji wa ndani na nje ya nchi pamoja na kuwa na vigezo na mambo muhimu ya kupakia (Requirements) kwa Waandishi wa Habari wa nje ya Tanzania.

Sambamba na hayo, mfumo huo utakuwa na uwezo wa kuhakiki taarifa za Waandishi wa Habari kwa kuunganishwa na mifumo mingine ya serikali kama GePG, NIDA, NECTA, uhamiaji na mifumo mingine kwa ajili ya malipo, uhakiki wa vyeti na taarifa (Verification).

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi