Na. Rodney Thadeus - MAELEZO, China
Aliyekuwa Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Lu Youqing akiongea katika majadiliano ya kibiashara baina ya wafanyabiashara wa Tanzania na China ambayo yalienda sambamba na maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Canton jijini Guangzhou, China.
Jina la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli limekuwa gumzo hapa nchini China kutokana na Serikali yake kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.
Aliyekuwa Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Lu Youqing pamoja na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wa China ambao wanataka kuwekeza nchini Tanzania, wamemuelezea Magufuli kama Rais aliyeonesha ushujaa kupambana na rushwa ambayo imekuwa ni tatizo kubwa miongoni mwa nchi za Afrika.
Rais Magufuli alielezewa katika majadiliano maalum yaliyoandaliwa kuwakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na China kujadili fursa za kibiashara, ikiwa ni sehemu ya Maonesho ya Kimataifa ya Canton yaliyofanyika katika jiji la Guangzhou nchini China.
“Tangu Rais Magufuli aingie madarakani kuna mambo makubwa yamefanyika katika mapambano dhidi ya rushwa. Serikali ya China itaendelea kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli kupambana na rushwa,” alieleza Balozi Lu Youqing.
Baadhi ya wafanyabiashara kutoka Tanzania wakifuatilia mada katika mkutano wa kujadili fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji baina ya wafanyabiashara wa Tanzania na wale wa China wakati wa maonesho ya Kimataifa ya Bisashara ya Canton yaliyomalizika hivi karibuni jijini Guangzhou, China.
Balozi Lu alieleza wazi kwamba msimamo wa Rais Magufuli wa kutovumilia vitendo vya rushwa, utajenga misingi imara ambayo itasaidia Tanzania kutimiza malengo yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati wa viwanda ifikapo mwaka 2025.
Pamoja na kusifu juhudi zinazofanywa na Serikali kudhibiti rushwa nchini Tanzania, Balozi Lu amewaeleza wafanyabiashara wa China wanaotaka kuwekeza nchini kuwa Tanzania ni nchi yenye mazingira bora ya uwekezaji kutokana na uimara wa ukuaji wa uchumi ambao umekuwa ukikua kwa zaidi ya asilimia saba kwa mwaka na kuwa nchi inayoongoza kwa ukuaji wa uchumi Afrika Mashariki.
“Tanzania ni nchi yenye amani na utulivu wa kisiasa na kuleta matumaini katika uwekezaji. Napenda kuwashauri wafanayabiashara na makampuni yanayowekeza Tanzania kumuunga mkono Rais katika vita ya rushwa,” alieleza Balozi Lu huku akisisitiza kuendelezwa kwa ushirikiano uliopo kati ya nchi hizo mbili.
Balozi wa Tanzania nchini China akijadiliana jambo na aliyekuwa Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Lu Youqing walipokutanda jijini Guangzhou katika mkutano wa wafanyabiashara wa Tanzania na wale wa China kujadili firsa mbalimbali za biashara na uwekezaji.
Pia katika mkutano huo, Makamu wa Rais Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo wa China kwa nchi za Afrika (CAD Fund) ambao unasaidia makampuni kuwekeza Afrika, Wang Yong alieleza kuwa Tanzania ni nchi muhimu kwa uwekezaji miongoni mwa nchi za Afrika hasa katika kilimo, madini na nishati.
“Nazishukuru Serikali za Tanzania na China kupitia Balozi Kairuki na Balozi Lu kwa kuwezesha makampuni ya kutoka China kuwekeza nchini Tanzania,” alishukuru Yong.
Mkutano wa kibiashara kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na China ambao ulienda sambamba na Maonesho ya Kimataifa ya Canton katika jiji la Guangzhou nchini China, ulilenga kuwakutanisha wafanyabiashara hao na kufungua fursa mbalimbali za kibiashara huku Watanzania wengi walionekana kuvutiwa zaidi na biashara ya muhogo ambapo kampuni ya Sino Light International Holdings ilionesha nia ya kununua tani 100,000 za muhogo mkavu kutoka Tanzania kila mwezi.