Na WMJJWM, Tokyo Japan
Viongozi waandamizi kutoka nchini Tanzania wapo nchini Japan kwa lengo la kujengewa uwezo kuhusiana na masuala ya ugatuaji wa Madaraka na namna nchi hiyo ilivyoweza kufanikiwa kwenye dhana hiyo kwa vitendo, hali itakayoziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa hapa nchini kujitegemea kimapato sambamba na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Akizungumza katika ziara hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Zainab Chaula, amesema wakiwa katika nchi hiyo ambayo imeonesha kuwa na mafanikio katika dhana hiyo ya Ugatuaji wamefanikiwa kutembelea Mji wa Oita, ambao ni maarufu kwa kauli mbiu ya "One Village One Product" hali iliyowawezesha wananchi hao kujikwamua kiuchumi.
“Sisi kama Makatibu Wakuu, tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wetu, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwani katika dhana ya kuwajengea uwezo, tumefanikiwa kuja hapa tukiwa Makatibu Wakuu wanne kutoka Wizara za Kisekta sambamba na Wakuu wa Mikoa lakini pia Wakurugenzi kutoka baadhi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, hii kwetu ni fursa na tutahakikisha tunatimiza malengo yaliyotuleta kwa manufaa ya nchi yetu”, alisema Dkt. Chaula.
Wakiwa nchini Japan, viongozi hao pamoja na mambo mengine wamefanikiwa pia kukutana na Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mhe. Baraka Luvanda na kufanya naye mazungumzo, ambapo katika mazungumzo yao viongozi hao wamesema matokeo ya ziara hiyo ni ushirikiano mzuri baina ya nchi hizo mbili wa muda mrefu na watatumia ziara hiyo kama shamba darasa.
Ziara hiyo ya kikazi imejumuisha Makatibu Wakuu wanne kutoka Ofisi ya Rais -Utumishi, Dkt. Laurian Ndumbaro, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. John Jingu na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Zainabu Chaula, wengine ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Ndugu Laurance Mafuru, Makatibu Tawala wa Mikoa ya Simiyu na Kigoma pamoja na Wakurugenzi Makamishna, sambamba na Wakurugenzi wa Halmashauri za Sumbawanga, Nanyumbu na Babati.