Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Viongozi wa Taasisi Waahidi Kutekeleza Maagizo ya Katibu Mkuu Kiongozi
Jul 15, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na. Georgina Misama – MAELEZO

Viongozi mbalimbali wa Serikali wameahidi kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga katika mafunzo ya siku mbili kwa Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala wa Mikoa pamoja na Naibu Makatibu Wakuu yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo uliwapa nafasi viongozi kujadili na kutathmini utendaji kazi serikalini, kupata mafunzo kutoka kwa wataalamu akiwepo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, wataalamu wa Sensa ya Watu na Makazi pamoja na kupokea maagizo ya kiutendaji kutoka kwa Balozi Kattanga.

“Mkutano huu ni wa tathmini ya utendaji kazi Serikalini na kuangalia namna bora ya kuweza kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kuwahudumia wananchi, tunamshukuru sana Katibu Mkuu Kiongozi tumepokea maagizo yake, tumejifunza mambo mengi na tumeweka maazimio ambayo yatapelekwa Wizarani na kushushwa kwenye Taasisi kwa ajili ya utekelezaji,” alisema Masanja Kadogosa, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC).

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Hassan Abbas Rungwe alisema kikao hicho kilikuwa muhimu kwa viongozi kwa lengo la kuongeza ufanisi kwenye utendaji na usimamizi mzuri kwenye rasilimali za nchi ambapo matarajio ni kwamba wananchi watapata huduma nzuri kwa wakati na kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

“Tumepokea maelekezo, kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Husein Katanga kwamba twende tukaimarishe usimamizi wa rasilimali na tusisite kuchukua hatua za kisheria na kinidhamu dhidi ya watendaji wote watakaobainika kufanya ubadhilifu wa mali za Umma, tupo tayari kwenda kuyatekeleza,” alisema Rungwe.

Akifunga mafunzo hayo Balozi Kattanga aliwataka viongozi wote kutambua nafasi zao kama watendaji wakuu na wasimamizi wa shughuli za serikali na kuwasisitiza kwamba wana wajibu wa kuhakikisha kuwa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi 2022 linafanyika kwa ufanisi na mafanikio kama ilivyokusudiwa na Serikali.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi